Viroba vyaweka kura rehani -VIDEO

Viroba vyaibukia Bungeni, Masaju aunguruma

Muktasari:

Wafanyabiashara kadhaa ambao walikuwa na viroba hivyo katika maghala wamezuiwa kuuza, hivyo kuendelea kusubiri hatima ya mizigo hiyo kutoka kwa Serikali. Pombe hizo za viroba zilipigwa marufuku nchini tangu Machi mwaka huu.

Dodoma. Katika zuio la Serikali la kupiga marufuku uuzaji wa pombe kwenye plastiki maarufu viroba likifanikiwa, linaonekana kuweka rehani kura za wabunge huku wakihaha kuangalia namna bora ya kuwasaidia wafanyabiashara hao.

Wafanyabiashara kadhaa ambao walikuwa na viroba hivyo katika maghala wamezuiwa kuuza, hivyo kuendelea kusubiri hatima ya mizigo hiyo kutoka kwa Serikali. Pombe hizo za viroba zilipigwa marufuku nchini tangu Machi mwaka huu.

Jana, katika hotuba yake ya bajeti, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamo Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema ofisi yake iliandaa kanuni za kusitisha matumizi ya vifungashio vya plastiki vya pombe kali ambalo lilichapishwa katika tangazo la Serikali namba 76 la Februari.

Wakizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, baadhi ya  wabunge waliitaka Serikali kutafuta namna ya kuwasaidia wafanyabiashara wa viroba ambao walilipa kodi kwa bidhaa hizo kuepuka hasara.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Hillary Aeshi alisema wafanyabiashara hao walikuwa halali, lakini namna ambavyo operesheni hiyo ilivyoendeshwa  itawasababishia hasara.

Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dallay Kafumu alisema njia bora ilikuwa ni kuzuia uzalishaji wa bidhaa hiyo ambayo ingefanya  viroba kutoonekana mtaani bila kuwapa hasara wafanyabiashara.