Vita CUF kuhamia Zanzibar

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama wote kuwa tayari kulinda ofisi zote za CUF, kutoruhusu kufanyika kwa vitendo vya uvunjifu wa amani.

Muktasari:

  • Walisema kwanza, watafanya mazungumzo ya amani na viongozi hao kuwataka kuzihama ofisi za chama hicho na iwapo watakaidi, nguvu za kisheria zitatumika.

Zanzibar. Uteuzi wa wakurugenzi uliofanywa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba huenda ukahamishia mgogoro wa uongozi visiwani hapa baada ya viongozi wapya walioteuliwa kusema wanajipanga kuwaondoa ofisini viongozi waliovuliwa nyadhifa zao iwapo watagoma kuachia kwa hiari.

Walisema kwanza, watafanya mazungumzo ya amani na viongozi hao kuwataka kuzihama ofisi za chama hicho na iwapo watakaidi, nguvu za kisheria zitatumika.

Lakini wakati wateule hao wakisema hayo, Katibu Mkuu chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama wote kuwa tayari kulinda ofisi zote za CUF, kutoruhusu kufanyika kwa vitendo vya uvunjifu wa amani.

Septemba mwaka jana, aliporejea madarakani kutokana na barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Lipumba aliingia kwa nguvu katika ofisi za chama hicho Buguruni na tangu wakati huo, kundi linalomuunga mkono Maalim Seif halijakanyaga huko likiwa limeweka ngome Makao Makuu yake Mtendeni visiwani hapa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Nassor Seif alisema wateule hao wapya wameshakutana na kukubaliana kufanya kazi kwa mwendokasi.