Vita mpya yaibuka kati ya Nyalandu na Kigwangalla

Lazaro Nyalandu

Muktasari:

  • Dk Kigwangalla jana alitumia mjadala wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2018/19, kushusha tuhuma nzito dhidi ya Nyalandu, ambaye muda mfupi baadaye alitoa waraka mrefu kupinga hoja hizo, akisema ni za kiasiasa zinazolenga kumchafua baada ya kuihama CCM na kudokeza kuwa familia yake inatishwa.

Dodoma. Ni kama vita mpya imeibuka; Dk Hamisi Kigwangalla, ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, na mtangulizi wake, Lazaro Nyalandu.

Dk Kigwangalla jana alitumia mjadala wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2018/19, kushusha tuhuma nzito dhidi ya Nyalandu, ambaye muda mfupi baadaye alitoa waraka mrefu kupinga hoja hizo, akisema ni za kiasiasa zinazolenga kumchafua baada ya kuihama CCM na kudokeza kuwa familia yake inatishwa.

Licha ya kukatizwa mara kwa mara na sauti za kuomba mwongozo na kutoa taarifa za kumtaka ajikite kujibu hoja zilizoibuliwa katika mjadala wa mpango huo, Dk Kigwangalla aliendelea na hoja yake akisema ameamua kufukua kaburi moja la mawaziri wa zamani, akiagiza Takukuru na Jeshi la Polisi vimchunguze waziri huyo wa zamani.

Ndani ya Bunge ilikuwa kama mashindano kati ya wabunge wa CCM na mawaziri waliokuwa wakipiga makofi kumuunga mkono Kigwangalla, huku wa upinzani wakiguna na kupaza sauti na kusababisha Mussa Zungu, aliyeongoza kikao hicho, kulazimika kutumia ukali kutuliza.

“Waheshimiwa order, order, order (utulivu). Hebu vumilieni. We (mbunge wa Mbozi, Pascal) Haonga kaa kimya. Huwezi kujibizana na kiti. Kaa kimya tulia,” alisema Zungu.

Baadaye alitumia kauli iliyovuma katika siku za karibuni iliyotolewa na mtu aliyejitokeza kununua nyumba za Said Lugumi.

“Itapendeza ukitulia,” alisema Zungu.

Wakati fulani, Kigwangalla alionekana kuchukia na kulazimika kuelezea tabia yake.

“Kuna watu wanaguswa na kuna watu hawaguswi. Mimi ni katika watu wasioguswa na sipendi mambo ya kipuuzi. Mimi huwa sichezewi chezewi,” alisema Dk Kigwangalla.

Akitoa tuhuma hizo, Dk Kigwangalla alisema hakusudii kufukua makaburi ya mawaziri waliomtangulia aliowataja kuwa ni Profesa Jumanne Maghembe, Ezekiel Maige na Balozi Khamis Kagasheki, bali Nyalandu.

Maige aliachia ngazi baada ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kuibua uozo katika wizara hiyo, huku Kagasheki akiondoka baada ya Kamati ya Bunge kubaini ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza iliyolenga kupambana na ujangili.

Profesa Maghembe aliachwa katika mabadiliko ya mwisho ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli.

Dk Kigwangalla alisema Nyalandu alikuwa akisemwa wabunge wa upinzani, kama mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, kuwa hatulii ofisini.

“Walisema Nyalandu kazi yake ni kustarehe kwenye mahoteli ya kitalii. Kazi yake ni kutembea nchi za mbali huko Marekani na warembo. Wakasema alienda Marekani na Aunt Ezekiel.”

Dk Kigwangala alisema Nassari aliwahi kuzungumza bungeni kuwa kama Dk Slaa angeshinda urais na kumpa uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa siku moja, angeanza kushughulika na Nyalandu.

“Leo naeleza kwa nini Nasari alikuwa sahihi kwa sababu wakati Nyalandu akistarehe katika hoteli ya Serena pale Dar es Salaam. Mezani kwake kulikuwa na GN ya tozo za mahoteli ya kitalii,” alisema.

Dk Kigwangwala alisema wakati Lazaro aliwahi kupewa chumba katika hoteli moja ambacho alikuwa anakitumia kama ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

Lakini mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali aliomba utaratibu kwa mwenyekiti akisema hoja iliyopo mezani ni kujadili Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2018/2019 uliowasilishwa Dk Mpango.

“Tunamuomba ajibu hoja za wabunge zilizoelekezwa kwenye wizara yake. Haya anayotuambia ya Nasari sisi humu ndani hatuyajui wala hatujayajadili wala hayakujadiliwa katika Bunge la 11,” alisema.

Lakini alipopewa nafasi, Kigwangalla aliendelea na ajenda yake, akisema Nyalandu hakusaini GN hiyo hadi alipondoka katika wizara hiyo na kuisababishia Serikali hasara ya takribani Sh32 bilioni kwa miaka miwili 2014 na 2015.

“Mambo kama haya ukiniambia nafukua makaburi mniache nifukue,” alisema Kigwangala na kuongeza kuwa lazima ajue ni kwanini hakusaini na alikuwa anashirikiana na nani wizarani.

“Mawaziri watakaoteuliwa pale wataendelea kutolewa tu na kukalia kuti kavu. Mie siko tayari kukalia kuti kavu na hata nikikaa miezi mitatu tu kwenye kiti nitakuwa nimeinyoosha hii sekta,” alisema.

Dk Kigwangalla alisema tuhuma ya pili ni mahusiano ya kutatanisha na bilionea wa Marekani anayemiliki makampuni matatu nchini, mojawapo ikituhumiwa kujiusisha na ujangili.

“Moja ya hayo makampuni ni Mwiba Holding, nyingine ni Windrose na nyingine Tanzania Game Tracker Safaris (TGTS). Kampuni ya TGTS ilipewa vitalu zaidi ya vile ilivyotakiwa kupewa,” alisema.

“Hapo kuna mambo ya kutatanisha. Lazima nijue kwanini walipewa vitalu zaidi. Kwa nini wanaendelea kuwinda. Kampuni ya Mwiba Holding ina tuhuma za ujangili.

“Kwamba inawinda kwa utalii lakini ilikamatwa na nyara za Serikali na hizi kampuni zinamilikiwa na mtu mmoja anaitwa Tony Flinking ambaye ni rafiki wa Nyalandu.”

Alisema Nyalandu alikuwa akitumia helkopta ya bilionea huyo wa Marekani kwa shughuli zake za uwaziri, kampeni za kugombea urais 2015 na shughuli za jimboni kwake.

Lakini Nyalandu, ambaye alikuwa waziri kamili wa wizara hiyo kwa takriban mwaka mmoja, hakuacha tuhuma hizo zipite.

Katika taarifa yake aliyoitumia Mwananchi jana, Nyalandu alisema inasikitisha kuona Dk Kigwangalla akitumia muda wa Bunge kumchafua, kudhihaki, na kusema, uzushi  na  uongo dhidi yake. 

Nyalandu, ambaye alisema yuko tayari kuchunguzwa na vyombo vya dola kwa sababu vipo kisheria, alisema kauli hiyo ni njama dhidi yake baada ya kuihama CCM.

“Hatua hii imepangwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi yeyote wa CCM atakayethubutu ama kudiriki tena kuhama CCM,” alisema Nyalandu.

 Alitoa hoja sita kuthibitisha kuwa Dk Kigwangalla anatumika vibaya, akianzia na hoja ya kusafiri kwenda nje na muigizaji filamu, Aunt Ezekiel, kuwa ni uzushi. 

“Habari ilikuwa ya kuzushwa  na ilichunguzwa na vyombo vya dola mwaka  2014 na kuthibitika ilitungwa,” alisema.

Alisema katika mkutano uliofanyika Washington DC, alialikwa na  Balozi wa Tanzania nchini Marekani na akapewa ruhusa ya maandishi na Serikali kuhutubia. Alisema Aunt Ezekiel na wasanii wengine hawakuwa na mwaliko wa Wizara ama Serikali, bali waandaji wa Kongamano.

Kuhusu helikopta, Nyalandu alisema Kigwangalla alipaswa kujiridhisha na kabla ya kuzungumza bungeni.

Alisema katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM, alitumia usafiri wa magari au ndege za kawaida hadi mchakato ulipoisha.

Alisema katika kampeni za ubunge, amekuwa akitumia helikopta kumalizia mikutano yake.

“Inawezekana Waziri Kigwangalla hajawahi kupanda helikopta katika maisha yake, nimjulishe tu kuwa kwangu huo ni usafiri wa kawaida sana,” alisema.

Kuhusu kutosaini tozo mpya alishalitolea ufafanuzi na baadaye kuandikiwa GN.

Kuhusu  vitalu,  Nyalandu  amesema Kigwangalla amelihadaa Bunge kwa kuwa mara ya mwisho vitalu vilitolewa Januari, 2017 wakati wa Waziri Maghembe na kabla ya hapo viligawiwa mwaka  2013 wakati wa Waziri Maige

“Hii ni aibu sana. Natumaini kwa Dk  Kigwangalla na wanaomtuma wangetamani sana miaka ibadilike ili isomeke Waziri Nyalandu,” alisema

Kuhusu kupewa chumba Hoteli ya Serena, Nyalandu alimtaka waziri huyo athibitishena kutaja namba ya chumba.

“Nilifanya kazi katika ofisi yangu iliyopo Wizara ya Maliasili na Utalii. Kigwangalla pia akumbuke mimi nilikuwa mteule wa Rais ambaye alikuwa na vyombo vya kumsaidia kusimamia mawaziri,” alisema.

Nyalandu alisema mbwembwe hizo za Kigwangalla zinatokana na uamuzi wake wa kuihama CCM.

Awali mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga aliomba kumpa taarifa Kigwangala, akisema kama Nyalandu alikuwa na uovu kiasi hicho alipaswa kuchukuliwa hatua kwa kupelekwa mahakamani muda mrefu badala ya kusubiri ahame CCM.

Mbunge mwingine wa Chadema, Sophia Makagenda akimtaka Kigwangalla pia apeleke bungeni taarifa za Maige na Profesa Maghembe.

“Wote kwa pamoja atupatie ili atusaidie ili Taifa letu lisonge mbele,” alisema Mwakagenda.

Habari zaidi na Bakari Kiango