VIDEO: Vitisho vyamng'oa Sanga Yanga

Muktasari:

Sanga alisema aliingia kwenye uongozi wa Yanga kwa mapenzi yake 


Makamu mwenyekiti wa Yanga, Injinia Clement Sanga la amejiuzulu wadhifa wake kutokana na vitisho anavyoendelea kupata kutoka kwa baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Protea, Osterbay jijini, Sanga alisema hawezi kuendelea kuongoza klabu hiyo huku yeye sambamba na familia yake wakiwa wanapewa vitisho vya kuuwawa kwa sababu ya nafasi yake.

"Hili suala nimelitazama kwa jicho la mbali zaidi. Imefika hatua mtu anazungumza bila kificho na kuhamasisha watu waje nyumbani kwangu wakiwa na mapanga, majembe na mashoka utadhani Sanga ana shamba wanakuja kunisaidia kulima.

Katika hali ya kushangaza, vitisho na taarifa hizi zimekuwa zikitolewa hadi kwenye magrupu ya mitandao ya kijamii ambayo mimi mwenyewe nipo lakini sioni watu wakikemea hadi napata hisia kwamba pengine kuna watu wapo nyuma ya hili.

Kutokana na hilo, nimeamua kujiuzulu kwa sababu tunaweza kulipuuzia hili likaleta matatizo siku za usoni," alisema Sanga.

Sanga alisema aliingia kwenye uongozi wa Yanga kwa mapenzi yake kwa klabu hiyo na wala sio tamaa ya fedha hivyo hataki kuondoka vibaya na kuchafua taswira yake na familia siku za usoni.