Viuatilifu feki vyawatesa wakulima

Muktasari:

  • Mtandao huo ulidai kwamba uingizwaji wa viuatilifu feki, umekuwa ukiwasababishia wakulima hasara kubwa.

 Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoa wa Arusha (Mviwata), umeiomba Serikali kudhibiti uingizwaji wa viuatilifu feki unaofanywa na baadhi ya mawakala wa pembejeo nchini.

Mtandao huo ulidai kwamba uingizwaji wa viuatilifu feki, umekuwa ukiwasababishia wakulima hasara kubwa.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Mviwata Mkoa wa Arusha, Richard Sakaya kwenye mkutano mkuu uliofanyika mjini hapa.

Sakaya alisema kumekuwapo na uingizaji mkubwa wa viuatilifu feki unaofanywa na baadhi ya mawakala, ambao umekuwa ukichangia hasara kubwa kwa wakulima.

Alisema tatizo hilo limekuwa likichangiwa na mawakala wengi kutojua matumizi sahihi ya viuatilifu hivyo, kutokana na kutokuwa na elimu ya utambuzi wa feki na halisi.

Akichangia hoja hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Mviwata Taifa, Hans Luwanja alisema kuwa licha ya tatizo hilo pia kuna ukosefu wa wataalamu wa kudhibiti.

Luwanja aliomba kuwapo kwa wataalamu wa kutosha katika ngazi za vijiji ambao watawezesha kudhibiti kwa karibu hali hiyo, ambayo inawafanya wakulima kupata hasara kubwa.

Naye Bwana Shamba Mkoa wa Arusha, Gaspar Urio aliwataka wakulima kujiunga katika vikundi ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutafuta masoko na pembejeo.