Viwanda, mashine suluhisho tatizo la ajira nchini - Waziri

Muktasari:

Dk Mpango aliyasema hayo jana alipotembelea banda la Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), kwenye maonyesho ya viwanda yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema ili kuhakikisha tatizo la ajira linapungua, Tanzania haina budi kuanzisha viwanda na mashine zitakazotoa ajira za moja kwa moja.

Dk Mpango aliyasema hayo jana alipotembelea banda la Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), kwenye maonyesho ya viwanda yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Maonyesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, yalianza Desemba 7, mwaka huu na yanatarajiwa kufikia tamati leo.

“Nimeona mashine zinazozalisha sabuni, mkaa na kusaga nafaka, hizi zote zinaweza kutoa ajira ya moja kwa moja kwa wananchi kama watazitumia vizuri. Mfano hii mashine ya sabuni mtu anatengeneza na kuuza sabuni hana haja ya kusubiri ajira ya Serikali,” alisema Dk Mpango.

Alisema kupitia viwanda na mashine hizo, pato la mtu mmoja mmoja na nchi litaongezeka kutokana na mzunguko wa bidhaa utakaokuwapo.

Kadhalika, Mpango alivutiwa na ubunifu uliofanywa na vijana mbalimbali katika banda hilo ambao wanatumia malighafi za hapa nchini kuzalisha bidhaa mbalimbali.

“Mmeonyesha mfano mzuri kwa vijana wasiotaka kubweteka bila kazi, badala yake mmetumia ubunifu wenu kufanya kazi kwa vitendo na tunaona matokeo yake. Serikali itawaunga mkono pale mtakapohitaji msaada,” alisema Dk Mpango.

Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji wa Sido, Janeth Minja alisema tayari wameanza kutengeneza mashine hizo kupitia wabunifu mbalimbali na zinazalisha ajira kwa asilimia kubwa.

“Kuna mashine ya kuchoma maandazi ambayo huchoma maandazi 240 kwa saa na inatumia gesi na nyingine inaumua mikate 140 kwa saa moja, hivyo inamfanya mwananchi ajiajiri mwenyewe,” alisema Minja.

Alisema zipo pia mashine za kusaga nafaka za aina zote, kutengeneza mkaa na baadhi ya bidhaa kama mafuta ya kula yanayotokana na malighafi za ndani.