Viwanda vya dawa vifuate utaratibu

Muktasari:

  • Serikali ipo bega kwa bega na TPI ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini

 Serikali kupitia Wizara ya Afya imevitaka viwanda vya kutengeneza dawa kufuata taratibu, masharti pamoja na kukidhi vigezo vya utengenezaji wa dawa zenye viwango kwa matumizi bora ya binadamu.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alisema hayo jijini Arusha alipotembelea kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu cha Tanzania Pharmaceutical Industry (TPI).

Alisema Serikali ipo bega kwa bega na TPI ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini, lakini inapaswa kufuata taratibu na masharti yaliyopo.

“Serikali haina budi kuipa ushirikiano TPI kuwasaidia kuboresha utengenezaji wa dawa nchini ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 80 iliyopo na kupiga hatua zaidi,” alisema Dk Ndugulile.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TPI, Zarina Madabida alisema kiwanda kipo katika hali nzuri ya kuzalisha dawa muhimu ili kuondokana na changamoto za upatikanaji wa dawa nchini.

“Tumeanza kuzalisha dawa za maji (syrup) na kuwafikia Watanzania, kupitia MSD (Bohari Kuu ya Dawa) ila mpaka kufikia Januari 2018 basi tunaamini tutapiga hatua kubwa zaidi,” alisema Madabida.

Dk Ndugulile pia alipata nafasi ya kutembelea Kituo cha Afya cha Nduruma kujionea hali ya utoaji huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hicho na uboreshaji wa miundombinu.

Dk Ndugulile alisema kituo hicho kimepiga hatua ya utoaji wa huduma za afya kwa kuwa kina dawa zote muhimu kwa asilimia 85 na wametumia vizuri Sh500 milioni walizopata kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya dawa, vifaa tiba na ukarabati wa kituo chao.