Viwanda vyapukutika mkoa wa Mara

Muktasari:

Viwanda vilivyofungwa ni vya Mara Milk Ltd (maziwa), Musoma Textile Mills Ltd (Mutex - nguo) na Prime Catch Exporters (samaki). Kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Musoma Fish processors Ltd (MuFPL) ndicho pekee kinaendelea, lakini uzalishaji wake ukiwa chini ya uwezo halisi.

Musoma. Shughuli za uwekezaji katika mkoa wa Mara zimetatizika baada ya viwanda vitatu vikubwa vya kuzalisha maziwa, kutengeneza nguo na kuchakata samaki kufungwa mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali hali inayotishia maelfu ya ajira na Serikali kupoteza mapato.

Viwanda vilivyofungwa ni vya Mara Milk Ltd (maziwa), Musoma Textile Mills Ltd (Mutex - nguo) na Prime Catch Exporters (samaki). Kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Musoma Fish processors Ltd (MuFPL) ndicho pekee kinaendelea, lakini uzalishaji wake ukiwa chini ya uwezo halisi.

Kufungwa kwa viwanda hivyo kumeishtua Serikali. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Dk Adelhelm Meru alisema wanayafahamu matatizo yanayovikumba viwanda hivyo na walishazungumza kwa kina na wawekezaji hao kujua namna wanavyoweza kusaidiwa na waliwasihi wasivifunge kwa kuwa Serikali ya sasa inatatua changamoto zinazowakabili.

“Ni kweli viwanda hivyo vimefungwa lakini Serikali haifurahi kwa sababu mikakati yetu ni kuhakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi kwa ufanisi kabla ya kuanzisha vipya. Tayari mikakati ya kuvilinda vya sasa imeanza kutekelezwa,” alisema.

Dk Meru alisema Mutex walikuwa wanalalamikikia ushindani wa nguo zinazoingia nchini bila kulipiwa ushuru na gharama kubwa za uendeshaji kwa sababu ya umeme; Prime Catch Exporters ni ukosefu wa malighafi ya samaki kutokana na uvuvi haramu na Mara Milk ilikuwa kuhusu gharama za ushalishaji kutokana na umeme.

“Matatizo yote hayo yalikuwa ya zamani lakini Serikali ya Rais (John) Magufuli imeamua kujenga uchumi wa viwanda na sasa hakuna bidhaa zinazoingia bila ushuru, uzalishaji wa umeme umeongezeka kutoka Megawati 670 miaka michache iliyopita hadi Megawati 1,450 na tunadhibiti uvuvi haramu ili kuhakikisha samaki wanarudi, hivyo wawekezaji wasiwe na wasiwasi,” alisema Dk Meru.

Takwimu za NBS

Viwanda hivyo vitatu ni miongoni mwa vilivyorodheshwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) hadi Desemba mwaka jana na kuchangia kuufanya Mara kuwa mkoa wa pili kwa viwanda nchini. Mara unashika nafasi ya pili kwa viwanda Tanzania Bara ukiwa na viwanda 3,573 sawa na asilimia 7.1 nyuma ya Dar es Salaam unaoongoza ukiwa na viwanda 7,705 sawa na asilimia 15.2.

Takwimu za NBS zinaonyesha kuwa kati ya viwanda hivyo, asilimia 94.5 ni vidogo vinavyoajiri kuanzia mtu mmoja hadi wanne wakati asilimia 5.5 ni viwanda vya kati na vikubwa. Hata hivyo, baadhi ya vyenye uwezo wa kuajiri watu zaidi ya 50 vilivyopo Manispaa ya Musoma havizalishi tena huku vingine vikiwa zimefungwa ndani ya miezi mitano iliyopita kutokana na kukosa malighafi au gharama kubwa za uendeshaji.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini viwanda vidogo vinakua kwa kasi, lakini vikubwa vinapukutika. Kati ya vinne vikubwa, Musoma Fish Processors Ltd (MuFPL) ndicho kinaendelea huku viwanda vya Mara Milk Ltd, Mutex na Prime Catch Exporters vimefungwa kutokana na sababu mbalimbali.

Mmoja ya maofisa waandamizi wa kiwanda hicho, kinachomilikiwa na Mohammed Enterprises Ltd (MeTL) alieleza kuwa kiwanda hicho kilikuwa kikijiendesha kwa hasara hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea kukiendesha.

“Hatujui uamuzi wa mwekezaji ila kwa ufupi hatuna uhakika kama kiwanda kitafunguliwa tena,” alisema ofisa huyo ambaye aliomba asitajwe gazeti kwa vile si msemaji wa MeTL.

Kiwanda cha Mutex kilichopo mtaa wa Lwamlimi kata ya Bweri, Musoma Mjini kilianzishwa na Serikali mwaka 1980, lakini kilibinafsishwa kwa MeTL mwaka 2008.

Taarifa ya fedha na biashara ya Manispaa ya Musoma inaonyesha kiwanda hicho kilikuwa na uwezo wa kuajiri watu 400, lakini hadi Machi mwaka huu kilikuwa na wafanyakazi 100.

Wimbi la kufungwa viwanda vikubwa mkoani humo linawatia hofu vijana wengi waliokuwa wakitegemea ajira na ni changamoto kwa Serikali ya Rais Magufuli yenye mpango wa kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Maisha yanazidi kuwa magumu hapa mjini,” alisema Emmanuel Elias aliyekuwa anafanya kazi katika kiwanda cha Mutex.

“Kiwanda cha samaki kimefungwa, kile cha maziwa kimefungwa, cha magodoro kilifungwa kitambo, kiwanda cha makaratasi (Isopack 2000 Ltd) tulishakisahau kimebaki kuwa nyumba ya popo na hiki (Mutex) kilichokuwa kimesalia nacho ndiyo hicho kimefungwa,” alisema.

Emmanuel na wenzie zaidi ya 30 walikutwa wamejaa kwenye geti la Mutex wakisubiri malipo yao likiwa kundi la mwisho la wafanyakazi wa kiwanda hicho baada ya kumaliza mikataba ya kazi ya kuchakata pamba na kuambiwa shughuli zote za kiwanda hicho zimefungwa rasmi hadi itakapotangazwa tena.

Mkurugenzi wa Mara Milk, James Mathayo alisema waliamua kufunga kiwanda hicho mapema Julai mwaka huu baada ya kuelemewa na madeni ambayo yalichochewa na kutojiendesha kw a faida.

“Hatupo tena sokoni,” alisema Mathayo kwa masikitiko. “Tulikuwa na madeni mengi yaliyotubana sana hasa gharama za riba na hatukuwa tukipata faida kubwa.”

Mathayo alisema pamoja na kwamba walikuwa na madeni, ulipaji wake uliathiriwa na gharama kubwa za uendeshaji zilizochagizwa na msururu wa kodi na tozo kiasi cha kufanya wasipate faida ipasavyo ambayo ingesaidia kumaliza deni. Kiwanda hicho kilikuwa na uwezo wa kuajiri watu 80.

“Kabla ya kufunga kiwanda tulikuwa tunaishauri Serikali juu ya uwepo wa tozo na kodi nyingi zinazoumiza wafanyabiashara. Kila waziri akija husema ‘tumeyachukua’ lakini hakuna kinachofanyika…Hii inachochea rushwa,” alisema.

Meneja wa Kiwanda cha samaki cha Prime Catch Exportes Ltd,Irfan Jessa amesema,“Mazingira ya biashara ni magumu na pia hakuna malighafi ya kutosha. Kiwanda kilikuwa kinaendeshwa chini ya uwezo wake kwa asilimia 80…hivyo kulikuwa hakuna sababu ya kuendelea kuzalisha.”

Aidha, uzalishaji katika kiwanda cha Musoma Fish Processors kinachoajiri wafanyakazi 280 uko chini ya uwezo. Mhasibu mwandamizi wa kiwanda hicho, Willbald James alieleza kuwa uwezo wao ni kuzalisha hadi tani 25 kwa siku lakini kwa sasa wanapata tani 12 pekee ya samaki hali inayosababishwa na kukithiri kwa uvuvi haramu ziwani.

“Kutopatikana kwa samaki kunasababisha tuzalishe kwa gharama kubwa kwa kuwa matumizi ya umeme, mishahara, kodi vinabaki pale pale. Hii inatishia mustakabali wa shughuli zetu. Tukifunga leo ajira na kodi kwa Serikali zitatoweka,” alisema James.

 

Viongozi wa mkoa

Sifa ya Mara kuwa mkoa wa pili wa viwanda nchini hususani viwanda vidogo huku vikubwa vinafungwa unafanya Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Adoh Mapunda ashindwe kuamini takwimu husika.“Si kweli. Unataka kueleza kuwa Mara ina viwanda vingi kuliko Mwanza? Hapana,” alisema Mapunda.

Hata hivyo, alisema Serikali imeanza kutatua changamoto za ukosefu wa malighafi za pamba na samaki kwa kuweka mikakati maalumu ya kuzuia uvuvi haramu na kuanzisha kilimo cha mkataba.

“Serikali inafanya doria ya uvuvi haramu mchana na katika maeneo yote kupitia idara ya uvuvi. Wakuu wa wilaya wote wa wilaya zenye zilizozungukwa na ziwa wanashiriki operesheni na zaidi ya nyavu 3,000 zimeshakamatwa na kuteketezwa,” alisema.

Katika kilimo cha mkataba, Mapunda alisema wamehamasisha wananchi wajiunge kwenye vikundi vinavyowekeana mikataba na viwanda vinavyotumia pamba katika uzalishaji ili vinunue zao hilo wakati wa mavuno kwa kukata gharama za mkopo.

Hii, alisema itasaidia uhakika wa upatikanaji wa pamba katika viwanda na kuwanufaisha wakulima.

Mapunda alisema baadhi ya viwanda kama Mutex vilikuwa na mitambo ya teknolojia ya zamani ambayo ilikuwa ni ghali kuiendesha.

Kuhusu kufufua viwanda vya zamani, Mapunda alisema wanaendelea na mikakati na sasa wizara ya viwanda na biashara inafikiria kumnyang’anya mwekezaji wa shamba la Utegi kilipokuwa kiwanda cha maziwa ili apatiwe mwekezaji mwingine thabiti akiendeleze.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Fidelica Myovella amesema kufungwa kwa viwanda hivyo katika mkoa ambao NBS inaonyesha hadi Desemba mwaka jana ulikuwa na viwanda vinne vyenye uwezo wa kuajiri watu 50 hadi 499, ni pigo kubwa.

“Ni bahati mbaya viwanda vinafungwa sasa lakini sidhani kama vitaendelea kufungwa kwa kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha vinafanya kazi” alisema.

“Tunafanya uchambuzi wa kina juu ya kinachoendelea tujue matatizo ili kama ni tatizo la menejimenti au malighafi. Tunapambana na uvuvi haramu ili kuongeza upatikanaji wa samaki hivyo siku zijazo haitakuwa tatizo.”

Aliwasihi wenye viwanda wasifunge kwa kuwa Serikali inazidi kuimarisha mazingira ya biashara ikiwemo kutenga maeneo maalumu ya viwanda likiwemo la hekta 83.66 katika Manispaa ya Musoma. Mkoa pia una eneo maalumu la uwekezaji wa viwanda (EPZ) lililopo wilayani Bunda ambalo Mkurugenzi wa Mji wa Bunda, Janeth Mayanja alisema linafikia ekari 400.