Vurugu zatawala uchaguzi Ifakara

Muktasari:

Mashabiki hao walitaka kuvamia kituo hicho katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbasa, baada ya mawakala kutokubaliana na matokeo.

Ifakara. Polisi wilayani Ifakara  wamelazimika kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya mashabiki wa vyama vya siasa waliotaka kuvamia kituo cha kupigia kura cha Mbasa Mlimani.

Mashabiki hao walitaka kuvamia kituo hicho katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbasa, baada ya mawakala kutokubaliana na matokeo.  

Katika vurugu hizo askari Huruma Mkisi alijeruhiwa kwa kupigwa jiwe kichwani na mtu asiyefahamika na hivyo kupelekwa katika Hospitali ya Mtakatifu Francis ya Ifakara kwa ajili ya matibabu. 

Awali, mashabiki hao walianza kwa kulalamikia matokeo ya uchaguzi kucheleweshwa kutangazwa na hivyo kuwatilia shaka mawakala ambao walikuwa wakibishana kuhusu idadi ya kura walizopata wagombea wao. 

Akitangaza matokeo, msimamizi wa Uchaguzi huo Gaston Kaputa alimtaja mshindi  wa nafasi ya mwenyekiti wa Kijiji cha Kisawila kuwa ni Shaaban Salahange wa CCM  aliyepata kura 557 aliyefuatiwa na Odric Matimbwa (Chadema) aliyepata kura 528 huku mgombea wa NCCR-Mageuzi Bakari Mkungundile akiambulia kura mbili.