Vyakula kushusha mfumuko wa bei

Muktasari:

  • Baada ya kupanda mfululizo tangu Januari hali inatengamaa baada ya msimu wa mavuno kuanza.

Kushuka kwa bei za vyakula kwa siku za hivi karibuni, kumeelezewa kuwa kutapunguza mfumuko wa bei.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema kupungua kwa bei hizo ni neema kwa walaji kwani hata bei ya vitu vingine itashuka, hali itakayowawezesha kufanya mambo mengine kutokana na fedha inayookolewa kwenye chakula.

Baada ya mfumuko wa bei kupanda mfululizo tangu Januari ulipokuwa asilimia 5.2 mpaka asilimia 6.1 Mei, hali inatengamaa baada ya msimu wa mavuno kuanza. Mfumuko huo ulipanda zaidi Machi na Aprili ulipokuwa asilimia 6.4, kabla haujashuka mpaka asilimia 5.4 mwezi uliopita.

Wakati ukipanda, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilieleza hali hiyo inachangiwa na kupanda kwa bei za vyakula suala ambalo limeanza kuchukua sura mpya.

Kiroba cha kilo 25 cha unga wa sembe kilichokuwa kinagharimu Sh55,000 sasa hivi kinapatikana kwa Sh28,000. Kilo moja ya nyama ya ng’ombe ilikuwa inauzwa kwa Sh8,000, imeshuka hadi kati ya Sh4,000 mpaka 5,500.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboje alisema ni jambo zuri la kufurahiwa na walaji, lakini akatahadharisha kwamba linaweza kuleta athari hasa kwa wakulima kwa sababu watashindwa kupata kipato cha kuendeleza kilimo. “Wengi watakuwa na uwezo wa kupata chakula lakini kikishuka sana, watapata hasara kama gharama za uzalishaji zitakuwa kubwa kuliko mapato baada ya mauzo ya mazao yao,” alisema Profesa Semboje. Alisema kama Serikali itajiridhisha na uwapo wa chakula cha kutosha, itapendeza zaidi ikitoa kibali kuuza nje kwa watakaokuwa nacho cha ziada. Katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam, gunia moja la mahindi la kilo 100 linauzwa kati ya Sh100,000 hadi Sh140,000 wakati gunia kama hilo la maharagwe linauzwa kati ya Sh170,000 hadi Sh230,000. Bei imeendele akuwa hivi tangu Januari mpaka Julai hii.

Ofisa Mipango wa Soko la Kariakoo, Henry Rwejuna alisema kutoshuka kwa bei ya vyakula kunatokana na kukosa wateja wa mara kwa mara kwa bidhaa nyingine.