Vyakula vyaibiwa usiku

Muktasari:

Kutokana na hali hiyo, wakazi wa Kata ya Nyang’ombe wanalazimika kukesha usiku kulinda akiba yao ya chakula chao isiibwe.

Rorya. Wakazi wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara wamedai kuibuka aina mpya ya wizi wa vyakula nyakati za usiku.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wa Kata ya Nyang’ombe wanalazimika kukesha usiku kulinda akiba yao ya chakula chao isiibwe.

Tayari, Mkuu Wilaya ya Rorya, Simon Chacha ameomba tani 500 za nafaka kutoka Ghala la Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), zitakazouzwa kwa bei nafuu ili kukabiliana na njaa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyang’ombe, Nelson Nyitambe amesema kumeibuka tabia ya watu wasiojulikana kuvizia vyakula, hasa udaga (unga wa muhogo) vinavyoandaliwa kwenye maeneo maalumu yenye miamba na kuondoka nao nyakati za usiku.

Mkazi wa Kijiji cha Ingri Juu, , Johnson Obande, ambaye ni miongoni mwa waliobiwa udaga uliokuwa ukiandaliwa kabla ya kuanikwa, ameiomba Serikali kuharakisha kupeleka msaada wa chakula cha bei nafuu kwa wananchi.

Hali ya chakula katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa ikidaiwa kuongezeka kutokana na ukame unaoyakumba maeneo hayo, huku ikidaiwa kuwa bei kwa sasa ni kubwa.