Vyama zaidi vyasusa kushiriki uchaguzi mdogo Desemba

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi

Muktasari:

  • Vyama hivyo vimesema chaguzi ndogo ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi, wazungumzia demokrasia kuminywa katika 'uwanja' wa uchaguzi

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza Desemba 2 ndiyo siku ya uchaguzi mdogo wa majimbo ya Serengeti, Simanjiro na kata 21 Tanzania Bara, vyama zaidi vya upinzani vimesusia kushiriki uchaguzi huo kwa madai ya kujua kinachokwenda kutokea.

Vyama hivyo ukiondoa Chadema ambao walisema muda mrefu kuwa hawatashiriki chaguzi ndogo, CUF na ACT Wazalendo bado wanajitathmini kama watashiriki au la, lakini vyama vingine navyo vimeweka wazi msimamo wao kuwa hawatashiriki.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, walibainisha kuwa wanajua kinachokwenda kutokea, hivyo hawana haja ya kujaribu demokrasia.

Katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema wana mtazamo tofauti na chaguzi alizoziita za mzaha zinazoendelea hapa nchini.

Alisema watu wanafanya wanavyotaka bila kujali wanawaumiza wananchi wanaokusanya kodi badala kuwaletea maendeleo inawaletea bughudha ya uchaguzi kila kukicha.

“Chaguzi ndogo ambazo tunaweza kushiriki ni zile ambazo mtu amefariki dunia au amepata matatizo ya akili, lakini hizi za kupangwa mtu anajiuzulu ubunge ili wagombee tena ubunge eneo hilo hilo, hatuwezi kushiriki,” alisema.

“Tumeshiriki chaguzi nyingine tumebakiwa na madeni na uwezo wa chama ni mdogo kwa sababu hatuna ruzuku, sasa badala tujipange kufanya vitu vya maana, tunaletewa chaguzi za ujanja ujanja, hatushiriki.”

Kauli ya Muabhi inaungwa mkono na katibu mkuu wa ADC Taifa, Doyo Hassan Doyo aliyesema kuwa hawashiriki kwa sababu wanaamini Tume ya Uchaguzi imekabidhiwa majukumu maalumu kuhakikisha hakuna jimbo wala kata yoyote itachukuliwa na upinzani.

“Kinachoonekana ikichukuliwa na upinzani mkurugenzi, mkuu wa wilaya hawana kazi kwa sababu walishapewa maelekezo, wanalipwa mishahara, wamepewa magari halafu watangaze upinzani watakiona,” alidai Doyo.

Alisema, “Hatuwezi kupeleka shingo huku tukijua tunakwenda kuchinjwa, tulishiriki uchaguzi wa Korogwe maneno yaliyokuwa yakisemwa na wanaowanadi wagombea ndiyo yaliyotokea.”

“Ndiyo maana baada ya uchaguzi wa udiwani Korogwe hatukushiriki uchaguzi wowote, wamteue mgombea wamtakaye na ikiwezekana wamtangaze mapema.”

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema hadi kufikia Ijumaa atatoa majibu kama wanashiriki chaguzi hizo ndogo au la. “Nipo jimboni Vunjo, kufikia Ijumaa nitakuwa na majibu ya kushiriki au kutoshiriki,” alisema.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema, “Mchezo huo nimeufahamu, siwezi kuchezeshwa bila ridhaa yangu nami nikacheza, nitakutana nao 2020.”

“Timu ya mpira ina wachezaji 11, kama refa, makamisaa, washika vibendera wote wao sasa unacheza mpira wa kazi gani si utafungwa, ”alisema.

Alisema ikifika 2020 jahazi litakuwa limezama hivyo watakutana majini kila mtu na lake akidai kuwa hivi sasa ubabaishaji umezidi.

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe alisema hawatashiriki kwa sababu umekuwa siyo uchaguzi isipokuwa ni vurugu na kwamba, wanawaachia watakaojitosa.

“Sina imani tena na sanduku la kura, tutasusia kushiriki chaguzi hadi watakapobadili tabia yao, sitaki kuwataja kina nani kwa sababu kila mtu anawajua,” alisema Rungwe.