Vyeti feki vilivyofyeka Sh50 bilioni za mabenki

Meneja wa Uzalishaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sameer Ahel akimuonyesha magazeti yanavyochapishwa, mkurugenzi mkuu na ofisa mtendaji mkuu wa NMB, Inene Bussemaker alipotembelea ofisi za Mwananchi, Tabata Relini jijini Dar es Salaam jana. Watatu kutoka kulia ni meneja wa kitengo cha Huduma kwa Jamii wa benki hiyo, Liliana Kisamba. Picha na Anthony Siame.

Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kuwaondoa watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki, imezifanya taasisi za fedha kutojua hatima ya Sh50 bilioni walizokopesha kwa watumishi hao.

Mkurugenzi mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana mara baada ya kutembelea ofisi za kampuni hiyo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Aprili 28, Rais John Magufuli alikabidhiwa orodha ya watumishi wanaokaribia 10,000 waliobainika kughushi vyeti na kuagiza waondolewe kazini bila kueleza hatima ya stahiki zao kama watapata au la.

Ineke alisema asilimia 90 ya watumishi hao walikuwa na mikopo katika benki zisizopungua sita ambao mpaka sasa hawajajua kama watazipata.

“Kwa kuwa Serikali haijatoa uamuzi wa mwisho juu ya watumishi hao, imani yetu tutaweza kuzipata, kwani asilimia 90 ya watumishi hao walioondolewa na Serikali karibia 10,000 walikuwa na mikopo katika benki mbalimbali ambayo inafikia kati ya Sh40 hadi Sh50 bilioni,” alisema Ineke.

Alisema NMB haijatetereka na deni hilo kwa kuwa hadi sasa ina kiwango kisichopungua Sh1.5 trilioni za kuwezesha kukopesha wateja wake.

Mei mwaka huu, waziri wa wakati huo wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki akijibu swali la nyongeza bungeni mjini Dodoma, alisema utaratibu utaandaliwa wa malipo yao na utakapokamilika watajulishwa na kulipwa stahiki zao.

Kairuki ambaye sasa ni waziri wa Madini alikuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Amina Mollel aliyetaka kujua ni hatua gani zitachukuliwa ili kuwalipa mafao yao wafanyakazi waliobainika kuwa na vyeti feki.

Sakata la wafanyakazi wenye vyeti feki limeendelea kuiumiza Serikali hususan katika eneo la mafao, kwani umekuwapo utetezi kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya wafanyakazi wanaotaka watu hao walipwe haki zao, ikiwamo mafao.

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) lilisema linaunga mkono watu hao walipwe haki zao za kiutumishi.

Katika mapambano ya rushwa, Ineke alisema ili vita hiyo iweze kufanikiwa ni lazima kukawapo na vyombo huru vya habari ambavyo vina waandishi waliobobea katika habari za uchunguzi.

“Ukiwa na waandishi wa habari za uchunguzi na vyombo huru vya habari vitasaidia sana kuibua masuala ya rushwa na hili limekuwa likijitokeza sehemu mbalimbali kwa waandishi kuibua kashfa kadhaa,” alisema Ineke

Kuhusu ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, mkurugenzi huyo mtendaji alisema ni muhimu ukawapo kwa kuwa ikitokea Serikali ikaacha kushirikiana na sekta binafsi, uchumi wa Taifa utayumba.

Ineke aligusia suala la mikopo katika eneo la kilimo biashara ambayo imeongezeka kwa sasa kutoka Sh40 bilioni miezi 18 iliyopita hadi kufikia Sh108 bilioni Septemba.

Alisema kwa sasa wanatoa mikopo hiyo katika sekta ndongondogo za kilimo 13 ambapo awali walikuwa wakitoa kwa wakulima wa mazao ya biashara tu.

“Tunatoa kipaumbele kwa kilimo biashara kuwapatia mikopo kwa sababu inachangia jitihada za Serikali katika kuijenga Tanzania ya viwanda na ndio maana mikopo yake imeongezeka hadi kufikia Sh108 bilioni,” alisema

Alisema licha ya changamoto kuwapo katika sekta ya kibenki kutokana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanywa na Serikali, ana matumaini kwamba kuanzia mwaka 2018 kutakuwa na unafuu kwa kuwa Serikali itaanza kuzitoa fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali.