Waandamana Uganda kutaka Mbunge Bobi Wine aachiwe

Muktasari:

Bobi Wine na wenzake sita wamefunguliwa mashtaka ya kutaka kuipindua Serikali ya Uganda


Kampala,Uganda. Jiji la Kampala jana liligeuka uwanja wa mapambano pale polisi na wanajeshi walipolazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kushinikiza kuachiwa kwa mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anayeshikiliwa katika gereza la Makindye.

Vurugu zaidi zilikuwa maeneo ya masoko ya Kisekkana na Namirembe pamoja na Kikuubo ambako waandamanaji walikuwa na mabango ya kutaka serikali imwachie Bobi Wine pamoja na mwenzake Francis Zaake.

Umati huo mkubwa ulikuwa ukishinikiza kuachiwa huru kwa wabunge hao pamoja na raia waliokamatwa wakidaiwa kushambulia kwa mawe na kupasua kioo cha moja ya magari katika msafara wa Rais Yoweri Museveni.

Walikuwa wameshika mabango ambayo yaliandikwa “nguvu ya watu, nguvu yetu” maneno ambayo huwa anapenda kuyatumia mbunge Bobi Wine.

Kamanda wa Polisi Dennis Nmuwooza amesema polisi wakishirikiana na wanajeshi walifanikiwa kuwakamata watu wengi waliokuwa kwenye maandamano hayo.

Museveni azima uvumi

Katika juhudi za kupoza hasira za wananchi, Rais Museveni alisema mbunge huyo hajajeruhiwa na amevishutumu vyombo vya habari akidai kwamba vinaeneza habari za uongo.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari, mbunge huyo ambaye pia ni msanii ana matatizo ya figo ambayo yanahitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea kutoa matibabu sehemu nyeti kama hizo za ndani ya mwili.

“Vyombo vya kueneza ‘habari za uongo’ vimekuwa vikitangaza kwamba mjukuu wetu, asiye na nidhamu Wine, ni mgonjwa mahututi, hawezi kuzungumza na mengineyo,” alisema Museveni

Aliongeza kwamba vyombo vya habari vilisema kwamba maofisa wa usalama wamemjeruhi vibaya kutokana na namna walivyokabiliana na wabunge wakati wakiwakamata.

Rais alisema tayari Bobi Wine alishapata matibabu kutoka kwa madaktari wa Arua, Gulu na Kampala na wamemuarifu kuwa hakuwa na majeraha ya kichwa, kifua wala mifupa kuvunjika.

Chama cha madaktari Uganda (UMA) kinasema mahali wanapohifadhiwa wabunge wa upinzani na vyombo vya usalama akiwemo Bobi Wine ni ya hatari na inaweza kuwasababishia kifo.

Viongozi wa chama hicho walisema madaktari wa Jeshi la UPDF hawana ujuzi wa kutosha kutoa matibabu kwa wabunge hao wanaodaiwa kujeruhiwa vibaya na maofisa wa usalama.

Rais wa chama cha Madaktari, Dk Edward Ekwaro Ebuku alisema ‘’Ugonjwa wa figo unatakiwa uangalizi wa dharura, jeshi la Uganda limemficha huyu Bobi Wine, isitoshe walimkataza Daktari wa familia kumtibu’’.

‘’Sasa hivi hatujui hali yake ikoje. Lakini tunafikiria wamemficha kwa sababu hali yake ni mbaya zaidi’’alisema

Wataalamu wa afya wanafafanua kuwa mtu akiwa na matatizo kwenye figo ni rahisi sana sehemu zingine kama maini na ubongo wake kuathirika iwapo hatua za dharura hazichukuliwi kumtibu.

Waliongezea kuwa mbunge Francis Zake ambaye ni miongoni mwa waliokamatwa yuko mahututi na anahitaji kuhamishwa kutoka hospitali moja hadi nyingine kupata matibabu ya hali ya juu.

‘Hatujapata ruhusa kuingia kambi za jeshi kuwaona wabunge hao, tutamuandikia mkuu wa jeshi Rais Museveni ili atupe ruhusa twende tumsaidie huyu mheshimiwa Robert Kyagulanyi’ alisema Ebuku.

Walia na serikali

Juzi mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na wengine watano kupata majeraha wakati polisi ilipokuwa ikizima maandamano ya wananchi wa Manispaa ya Mityana Magharibi mwa Kampala.

Vurugu hizo ziliibuka baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa mbunge wa upinzani Francis Zaake amekufa baada ya kupigwa na maofisa wa usalama anakoshikiliwa yeye na wenzake.

Raia wa Uganda wanaoishi nje ya nchi wameendelea kutuma ujumbe wa kuishtumu Serikali kwa vitendo vyake vya kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani na raia kwenye mitandao ya kijamii.

Mwanasheria wa mwanamuziki huyo alisema kwamba Bobi wine amechomwa sindano iliyomfanya asijitambue mpaka muda huu, na hata wanaomtembelea hawatambui wala uso wake hautambuliki huku masikio na pua zikitoa damu.