Waangalizi wasaka suluhu na timu ya Raila Odinga Kenya

Muktasari:

Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika, Thabo Mbeki alisema mgombea wa Nasa, Raila Odinga na ujumbe wake walikutana nao wakiwa na nyaraka za madai kuhusiana na Jubilee kuvamia kompyuta hizo.


Nairobi. Waangalizi wa kimataifa wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Madola wametoa ripoti zao za awali kuhusu uchaguzi Kenya na mazungumzo yao na kambi ya upinzani ya National Super Alliance (Nasa) iliyowasilisha madai kwamba kompyuta za Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ziliingiliwa na upande Jubilee ili kuvuruga matokeo ya kura.

Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika, Thabo Mbeki alisema mgombea wa Nasa, Raila Odinga na ujumbe wake walikutana nao wakiwa na nyaraka za madai kuhusiana na Jubilee kuvamia kompyuta hizo.

Mbeki alisema waliwasikiliza na kuwaeleza kuwa watalifikisha suala hilo IEBC. Hata hivyo, alisema Nasa walitaka waangalizi hao wazifanyie kazi nyaraka hizo.

“Kwa mtu kama sina utaalamu wa teknolojia kuniambia nichunguze ni sawa na kuniambia nifanye kazi ambayo sina ujuzi,” alisema Mbeki.

Aliongeza kuwa kazi ya waangalizi ni kuangalia ni sio kuchunguza kwa kuwa jukumu lao ni kuangalia namna mchakato ulivyofanyika iwapo ulifuata sheria za nchi na taratibu za kuheshimu demokrasia walizojiwekea katika Umoja wa Afrika.

Alisema tuhuma zote zilizotolewa na Nasa wameziwasilisha kwa mamlaka husika ndani ya Kenya.

Kwa upande wake, mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola, Rais wa zamani wa Ghana, John Mahama alisema walikutana na Odinga na ujumbe wake ambao walitoa madai ya kompyuta za IEBC kuvamia huku wakiwa na nyaraka kama ushahidi wao.

Hata hivyo, Mahama alisema nao waliwaeleza kwamba hawana utaalamu wa teknolojia hiyo, lakini jukumu lao ni kuangalia kama utaratibu wa uchaguzi ulifuata sheria na katiba ya nchi na madai mengine ya ukiukwaji wa taratibu yana utaratibu wake uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

 

Mwanafunzi awa mbunge

Aliyekuwa mgombea ubunge wa Igembe Kusini nchini humo, John Mwirigi (23) alishinda nafasi hiyo baada ya matokeo kutangazwa na IEBC.

Mwirigi ambaye anatajwa kuwa mbunge mwenye umri mdogo kuwahi kutokea aliwashangaza wengi katika kampeni ambapo alikuwa akitumia baiskeli na bodaboda.

Mbunge huyo mpya ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya alikuwa mgombea binafsi na hakuwahi kuwa na matangazo kwa kile kilichodaiwa ni kutokuwa na fedha za kufanyia kazi hiyo.

Katika matokeo hayo, Mwirigi alipata kura 18,867 huku mgombea wa Jubilee, Rufus Miriti akipata kura 15,411.

 

Wagombea wakubali matokeo

Aliyekuwa mgombea wa urais, Dk Ekuru Aukot amekubali kushindwa akifuatiwa na Dk Japheth Kavinga Kaluyu kukubali kushindwa juzi.

Dk Aukot alisema anaamini, “Wachache walipata fursa ya kusikika na wengi walishinda.”

“Jiwe la Daudi halikumuweza Goliathi wakati huu na asiyekubali kushindwa si mshindani.”

Licha ya kukubali kushindwa alitamka kuwa nchi hiyo isingekuwa na demokrasia bila ya Raila Odinga

Alimtaka Rais Kenyatta akitangazwa mshindi, aunde Serikali ya mseto na asiwabague wapinzani wake.

Pia, Dk Aukot alisema licha ya kushindwa kwake, lakini atawania tena urais mwaka 2022.

 

Nkurunziza ampongeza Kenyatta

Hata kabla ya matokeo rasmi ya uchaguzi nchini humo kutangazwa, Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alituma ujumbe wa kumpongeza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi katika akaunti ya Twitter.

 

Waangalizi wakubali

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema taarifa za awali za waangalizi wa uchaguzi wa nchini humo na wale wa nje, wote wanakubali kwamba uchaguzi ulikuwa wa wazi, huru na wa haki.

“Tumefanya kila tuwezalo kuhakikisha uchaguzi umekuwa huru na wa haki,” alisema.

Kiongozi wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU), Thabo Mbeki alisema shughuli ya upigaji kura nchini Kenya ilikuwa ya uwazi na waangalizi hao waliridhishwa na shughuli hiyo.

Hata hivyo alisema kulikuwa na changamoto kadhaa, mfano ingawa karatasi zilikuwa za rangi tofauti pamoja na masanduku, kulikuwa na rangi mbili ambazo zilikuwa zinakaribiana.

Hata hivyo, alisema maofisa wa uchaguzi waliwasaidia wapiga kura kutofautisha rangi hizo.

Mbeki aliipongeza pia Serikali na IEBC kwa kuhakikisha wafungwa wanapiga kura.

“Tunafahamu kwamba IEBC bado inahesabu na kukagua matokeo. Shughuli ya uchaguzi bado inaendelea, hivyo bado ni mapema. Hata hivyo, waangalizi wa AU wanafurahi kwamba uchaguzi ulikuwa wa amani, siku ya uchaguzi watu walifika kwa wingi na waliruhusiwa kupiga kura kwa kufuata taratibu za uchaguzi Kenya na zinazokubaliwa na AU,” alisema.