Wabunge 17 CCM waponea chupuchupu kutimuliwa

Muktasari:

Rais Magufuli amesema hata kama Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa naye angekuwamo katika kupinga mapendekezo ya Serikali, angetimuliwa.

Dar es Salaam. Sakata la korosho lililozua mjadala katika mkutano wa Bunge la Bajeti limemuibua mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli aliyesema walipanga kuwatimua uanachama wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara iwapo wangekwamisha Sheria ya Bajeti 2018.

Rais Magufuli amesema hata kama Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa naye angekuwamo katika kupinga mapendekezo ya Serikali, angetimuliwa.

Mjadala huo ulihusisha zaidi ya Sh200 bilioni za ushuru wa mauzo ghafi ya korosho nje ya nchi na mabadiliko ya sheria yaliyopendekeza fedha zote za ushuru huo kuingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Hatua hiyo iliwafanya wabunge wa mikoa ya Kusini kuungana na wanaotoka mikoa mingine inayolima korosho kuibana Serikali, huku baadhi ya wabunge wa CCM wakisema mabadiliko na kutolipwa kwa fedha hizo kutakiua chama hicho katika mikoa hiyo.

Majimbo ya mikoa ya Kusini yako 18, Mtwara ikiwa nayo 10 na Lindi manane, na CCM inaongoza kwa kuwa na majimbo 11 huku upinzani nayo saba. Ukijumlisha na wabunge wawili wa viti maalumu, mmoja wa Lindi na mwingine wa Mtwara wanakuwa 13 wa CCM.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu katibu wakuu aliowateua juzi, Rais Magufuli alimpongeza mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba aliyemwapisha kuwa naibu waziri wa Kilimo jinsi alivyochangia akiunga mkono mapendekezo ya Serikali.