Zuma kupigiwa kura ya kutokuwa na imani Alhamisi

Muktasari:

Kwa mujibu wa watu kutoka ndani ya kikao hicho, Spika wa Bunge, Baleka Mbete atapanga ratiba kuruhusu chama cha ya Economic Freedom Fighters (EFF) kuwasilisha bungeni hoja hiyo Alhamisi mchana.


Pretoria, Afrika Kusini. Kikao cha wabunge wa chama tawala cha African National Congress (ANC) leo kimepitisha uamuzi kwa kauli moja kuwasilisha hoja ya kupiga kura ya kukosa imani dhidi ya Rais Jacob Zuma siku ya Alhamisi.

Kwa mujibu wa watu kutoka ndani ya kikao hicho, Spika wa Bunge, Baleka Mbete atapanga ratiba kuruhusu chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kuwasilisha bungeni hoja hiyo Alhamisi mchana. Kisha hoja hiyo itafanyiwa marekebisho na wabunge wa ANC.

Vyanzo kutoka ANC vinasema ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Tandi Mahambehlala pekee aliyejaribu kuanzisha mjadala kuhusu jambo hili, lakini alipingwa na wabunge wenzake ambao ni wengi.

Kikao hicho kilifanyika katikati ya mvutano mkubwa wa kisiasa ndani ya chama chenye Serikali ambacho kimeshindwa kumshawishi Rais Zuma kuondoka ofisini kwa hiari.

Mhasibu Mkuu wa ANC, Paul Mashatile ndiye alihutubia kikao hicho siku ambayo watu watatu wanaotuhumiwa katika kashfa ya kuiweka Serikali mfukoni walikamatwa na polisi wa kitengo cha kupambana na ufisadi (Hawks).

Kikosi hicho cha Hawks kilivamia Jumatano asubuhi makazi ya familia ya Guptas ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinyoshewa kidole kwa tuhuma zinazomkabili Zuma za kuiweka Serikali mfukoni.

Awali kikao hicho kilipangwa kufanyika saa 4:00 asubuhi, lakini kilisogezwa hadi saa 5:00 kwa matarajio kwamba Zuma angehutubia Taifa saa nne.

Hata hivyo, baadaye ilitolewa taarifa iliyoonyesha kwamba Zuma bado hakuwa tayari kuutangazia umma. Kulikuwa na uvumi kwamba Zuma angeweza kutumia fursa hiyo kujiuzulu baada ya ANC kumpa onyo la mwisho.