VIDEO: Wabunge Komu, Kubenea wawasili kikao cha Kamati Kuu Chadema

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini (CHADEMA), Anthony Komu na Mbunge wa Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea wakiwasili eneo kinapofanyika  kikao cha kamati kuu ya chama hicho.

Muktasari:

Wakati  kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kikiendelea leo Jumatano Oktoba 17, 2018 wabunge wawili wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania, Saed  Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) wamewasili eneo kinapofanyika kikao hicho


Dar es Salaam. Wakati  kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kikiendelea leo Jumatano Oktoba 17, 2018 wabunge wawili wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania, Saed  Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) wamewasili eneo kinapofanyika kikao hicho.

Kikao hicho kinachofanyika katika ukumbi wa Ledger Plaza katika Hoteli ya Bahari Beach kinajadili masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chama hicho likiwamo la wabunge hao.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa ni sauti yao inayosikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hiyo kwa kile walichoeleza ni ya kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Leo saa 8:01 mchana Komu na Kubenea wameshuhudiwa na MCL Digital wakiwa nje ya ukumbi huo wakisubiri maelekezo ya kuingia katika kikao hicho.

Pia, Chadema kimeonyesha magari yake aina ya Ford Ranger ambayo yatatumika katika shughuli za kukiimarisha chama hicho na kukirejesha kwa wananchi.

Msemaji wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania, Tumaini Makene  ameseama magari hayo yatatumika katika chaguzi na utekelezaji programu ya Chadema msingi.