Wabunge Mtwara wakerwa kusuasua ujenzi wa hospitali

Katibu mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally akitoka kukagua ujenzi wa majengo ya hospitali ya rufaa kanda ya kusini yanayoonekana kwa nyuma.Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

  • Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa wamesema kuchelewa kwa fedha za  ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kumesababisha kusuasua kwa ujenzi huo

Mtwara. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa wamesema kuchelewa kwa fedha za  ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kumesababisha kusuasua kwa ujenzi huo.

Wameeleza hayo leo Jumamosi Septemba 22, 2018 walipofanya ziara kujionea ujenzi huo wakiwa pamoja na  Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally.

Wabunge hao wamesema kwa miaka mingi fedha zimekuwa zikitengwa lakini hazipelekwi.

Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia amesema zaidi ya miaka mitatu hospitali hiyo imekuwa ikitengewa Sh2 bilioni lakini hazitoki licha ya kuwa na ufuatiliaji.

“Kikubwa ni msukumo wa wizara yenyewe kwa sababu Serikali imejikita kuboresha sekta ya afya, inajenga vituo vya afya na hospitali nyingi za wilaya. Sasa waonee umuhimu wa hospitali ya kanda. Kama wabunge kazi yetu tumefanya sana,”amesema Ghasia.

Mbunge wa Nanyumbu, Dua Nkurua ameishukuru Serikali kwa kuwa na lengo la kujenga hospitali hiyo na kuomba iweke kipaumbele kutokana na sekta ya afya kuwa na umuhimu.

“Kama ujenzi huu utakamilika hospitali hii itakuwa mkombozi mkubwa  kwa wananchi wa kusini kwa sababu hivi sasa wanapata tabu ya kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine kusaka huduma, “ amesema.

Kwa upande wake Bashiru amesema mradi huo ni muendelezo  wa miradi ambayo chama hicho tawala kimepania kuitekeleza huku akiomba kupata maelezo kutoka kwa waziri husika kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo.

“Wabunge naomba mfuatilie kwa ukaribu mradi huu kupitia kwenye chama. Chama tuendelee kusimamia serikali ndio kazi yetu na sisi tuna maslahi kwa sababu ni wazo lililotokana na kikao cha halmashauri kuu ya Mkoa,”amesema

Kaimu mganga mkuu wa Mkoa wa Tabora,  Dk Alhaji Chibwana amesema makadirio ya ujenzi ya hospitali hiyo yaliyofanyika mwaka 2009 ambayo ni Sh75 bilioni na kwamba hadi sasa umeshagharimu Sh2.6bilioni