Wabunge machachari kwa hoja, misimamo wapotea

Muktasari:

Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge inaonyesha kuwa watunga sheria hao walipaswa kuwa mjini Dodoma tangu Jumapili iliyopita  kwa ajili ya vikao vya kamati. 

Dar es Salaam. Wakati mkutano wa Sita wa Bunge ukianza Januari 31 mjini Dodoma, wananchi watakosa kuwaona wabunge machachari waliotikisa Bunge la Kumi kwa hoja, vitimbi na misimamo mikali kupitia televisheni zao.

Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge inaonyesha kuwa watunga sheria hao walipaswa kuwa mjini Dodoma tangu Jumapili iliyopita  kwa ajili ya vikao vya kamati.

Hata hivyo, kwa wananchi, ambao sasa hawaoni tena matangazo yote ya shughuli za Bunge, hasa yale ya mijadala mikali, watakuwa wakikumbuka jinsi walivyokuwa wakiwaona baadhi ya wabunge machachari wakichachafya vikao kwa hoja zao.

Serikali ilitangaza kufuta matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya shughuli za Bunge, hasa vikao vya jioni ambavyo huhusisha mijadala ya miswada, masuala ya kitaifa na mambo mengine.

Baadhi ya wabunge machachari wa Bunge la Kumi lililoongozwa na Spika Anne Makinda ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye wakati huo alikuwa anawakilisha chama cha NCCR Mageuzi.