Wednesday, May 16, 2018

Wabunge waikomalia Serikali kushuka bei ya pamba, kamati yadai ripoti ya tume

 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Dodoma. Baadhi ya wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2018/19, wametaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu kushushwa bei ya pamba kwa kilo kutoka Sh1,200 hadi Sh1,100.

Mei Mosi, akiwa katika Kijiji cha Bukama wilayani Igunga, waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alitangaza kuwa, “bei ya pamba imeshuka kutokana na kuyumba kwa bei katika soko la dunia.”

Katika hali iliyoonekana ni nafuu kwa upande mwingine, Dk Tizeba alitangaza uamuzi wa Serikali wa kuwafutia wakulima wa zao hilo deni la Sh30 bilioni lililotokana na mkopo wa viuatilifu na kwamba, watalipa mkopo wa mbegu pekee.

Hata hivyo, jana, mbali na hilo, Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imetaka taarifa ya tume iliyochunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji iwasilishwe bungeni ili wabunge waijadili.

Hayo yalijiri bungeni mjini Dodoma jana, wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara hiyo iliyoomba kuidhinishiwa Sh170.2 bilioni kwa mwaka 2018/19 ambayo ni pungufu kwa asilimia 23 ikilinganishwa na ya mwaka 2017/18 ya Sh221 bilioni.

Wakichangia mjadala huo utakaohitimishwa leo, wabunge wa CCM, Richard Ndassa (Sumve) na Mashimba Ndaki (Maswa Magharibi) walisema hawawezi kuiunga mkono bajeti hiyo kwa kuwa haijaonyesha dhamira ya kweli ya kuwasaidia wakulima wa pamba.

Ndassa alieleza kuwa pamba ni siasa na ni uchumi akisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahamasisha wakuu wa mikoa 10 na wilaya 46 zinazolima pamba kuongeza kilimo. Alisema matarajio ya wananchi ilikuwa bei ya mwaka jana ya Sh1,200 ingeendelea, lakini sasa ni Sh1,100.

Ndassa alisema mkulima wa pamba anagharimia madeni asiyoyasababisha jambo linalokatisha tamaa na kutaka waziri wa wizara hiyo, Dk Tizeba atakapohitimisha bajeti yake leo kueleza kwa nini bei imeshuka. “Niwaombe wabunge wanaotoka maeneo wanayolipa pamba, tusiunge mkono ili kupata maelezo ya Sh1,100 ilikuwaje, Dk Tizeba mwakani kuna uchaguzi tutawaeleza nini wakulima wetu, wamehangaika, tunataka muirudishe hiyo Sh100,” alisema Ndassa.

Mbunge Ndaki alisema haungi mkono hoja iwapo bei ya pamba haitakaa vizuri. “Kuna mambo mengi yanasikika moja ni Sh33 zinabaki ushirika, Sh12 zinakwenda kuimarisha chama kikuu cha ushirika, Sh55 zinakwenda wapi? Ni muhimu sana tunapofika katika masuala yanayogusa watu wengi Serikali iwe sikivu” alisema. Ndaki alisema tangu msimu wa mauzo ya pamba ulipoanza Mei Mosi mpaka sasa hakuna iliyouzwa jimboni kwake na wala haifahamiki itauzwa lini kwa kuwa wananchi wamepoteza imani kwa vyama vya ushirika.

Mbunge wa Nzenga Mjini (CCM), Hussein Bashe alisimama kumpa taarifa Ndaki akisema, “baadhi ya vyama vya ushirika vimechagua viongozi wasiokuwa na ‘credibility’ katika maeneo hayo, hawaaminiki na wana historia mbaya, yaani kule wanaitwa ‘magaragaja.”

Maofisa ugani pia waliguswa katika mjadala huo na mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), Mahmoud Mgimwa aliyesema wanapaswa kuwajibika moja kwa moja kwa katibu mkuu wa wizara.

“Kwetu Mufindi debe la mahindi ni Sh3,000, halafu kilo moja ya sukari ni Sh3,000, yaani mtu akitaka kilo moja ya sukari auze debe moja? Nitawahamasisha wabunge wa Mufindi na wabunge wengine tuipinge kwani tunapigwa,”alisema.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Aida Khenani alisema wakulima wamefanywa kuwa maskini akieleza kuwa gunia la mahindi mkoani Ruvuma linauzwa Sh18,000 hali inayowafanya waishi maisha magumu.

Kamati yacharuka

Awali, akiwasilisha maoni ya kamati, makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Christine Ishengoma alisema migogoro baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi imekuwepo na kuathiri uzalishaji katika kilimo.

“Kwa kutambua hivyo na kuzingatia malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wabunge ambao kimsingi ndio wawakilishi wa wananchi, yalisababisha Serikali kuunda tume inayohusisha wizara tano zinazohusika na ardhi,” alisema Dk Ishengoma, huku akisisitiza taarifa ya tume iwasilishwe bungeni ili Bunge liweze kutekeleza wajibu wake wa kuishauri Serikali.

-->