Wabunge waja juu mauaji ya askari wanane

Spika wa Bunge Job Ndugai akizungumza bungeni mjini Dodoma. Picha na Maktaba

Muktasari:

Wataka Bunge lijadili hali ya usalama nchini

Dodoma. Wabunge wamekuja juu kuhusu sakata la mauaji ya askari wanane wakitaka Bunge liahirishwe ili kuruhusu kujadiliwa suala la usalama nchini.

Askari hao waliuawa na watu wasiojulikana Alhamisi wiki iliyopita wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Jana baada ya Bunge kurejea kutoka mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka baada ya kipindi cha maswali na majibu Dotto Biteko (Bukombe-CCM), Amina Mollel (Viti Maalum-CCM) na Joseph Kakunda (Sikonge-CCM) ambao walitaka Bunge liahirishwe ili Bunge lijadili kuhusu suala la usalama.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilikutana na mawaziri wawili wenye dhamana kujadili matukio ya kiusalama ikiwa ni pamoja na sakata la mauaji ya askari hao wanane.

Spika Ndugai alisema bungeni hayo jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu miongozo iliyotolewa na wabunge hao.

Akiomba mwongozo wake, Biteko alitumia kanuni ya 69 kuomba kutoa hoja ya kuahirisha Bunge ili kujadili suala la mauaji hayo.

Alisema Aprili 13 mwaka huu katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti waliuawa askari wanane na watu wasiofahamika.

“Askari hawa walikufa wakiwa wanatekeleza majukumu ya kutulinda sisi raia na mali zetu tukio hili si la kwanza Wilaya ya Kibiti liliwahi kutokea Februari 21, mwaka huu ambapo watu watatu waliuawa akiwamo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kibiti, Peter Kubeza,” alisema.

Alihoji kama askari hawapo salama kwa kiwango hicho raia wa kawaida hali yao si nzuri kwani jambo hilo limetokea Kibiti lakini linaweza kutokea Wilaya ya Kongwa linaweza kutokea Bukombe linaweza kutokea mahali kwingine kokote kama Taifa halijachukua hatua madhubuti.

Aliomba mwongozo kwa Spika ili suala hilo lijadiliwe ili Bunge litoe kauli kwa Serikali juu ya jambo hilo.

“Bunge lijadili ili kuondoa hofu wananchi maana kwa matukio haya yanayoendelea kutokea wana hofu kubwa juu ya usalama wao na maisha yao na mali zao juu ya matukio haya naomba tuahirishe Bunge tujadili suala hili,” alisema Biteko.

Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah alisisitiza kuwa suala hilo lijadiliwe na kumuomba Spika atumie busara ili suala hilo lipate nafasi.

Akijibu mwongozo huo Spika huyo alisema tayari kamati ipo kazini na kupitia kikao hicho Serikali itaeleza namna ilivyojipanga na itatoa maelezo ya namna ilivyojipanga kukabiliana na matukio mengine yanayoweza kujitokeza na kuhatarisha hali ya usalama ya polisi, raia na mali zao.

“Niungane na waheshimiwa wote mlioonyesha kuguswa sana na suala hili la askari wetu kiwango cha kufikia wanane wakati mmoja kuuawa kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana,” alisema.

Alisema kwa niaba ya Bunge zima anatoa pole na rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa jambo kubwa ambalo limeshtua nchini.

Alisema kamati hiyo inakusudia kukutana na mawaziri husika na baada ya kamati kulifahamu vyema jambo hilo ndipo Bunge litaweza kujadili.

“Baada ya kamati kulifahamu kwa undani wake na sisi tutaweza kulijadili lakini nashukuru tayari kamati imeshaanza kuchukua hatua,” alisema.

Aliwaomba wabunge kuwa watulivu na kwamba ameongea na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na amemhakikishia kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama wa nchi kwa sasa vipo kazini si kwenye maeneo hayo tu bali kwa nchi nzima.

“Kwa hiyo tuwape nafasi na kamati yetu ifanye kazi hii badala ya sisi wote kuifanya kwa sasa kama kamati itaona umuhimu wa jambo hili bado tupo tutapeana taarifa tunaweza bado tukarudi na tukalizungumza ikibidi hapa mbele,” alisema Ndugai.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kwamba Serikali inalichukulia tukio hilo kwa uzito mkubwa ili kuhakikisha kuwa wanarejesha hali ya usalama katika maeneo hayo.

Aliwatoa hofu wananchi na kusema kuwa tukio hilo limewapa chachu zaidi ya kupambana na uhalifu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira salama wao pamoja na mali zao.