Wabunge walia kukithiri uchafu nyumba wanazoishi

Muktasari:

Mbunge Joyce Mukya amesema wapangaji wamekuwa wakilipa kodi ya pango ya Sh150,000 na Sh250,000 kwa nyumba moja, lakini mazingira ya eneo hilo yamegubikwa na uchafu.


Dodoma. Wabunge wanaoishi katika maghorofa yanayomilikiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) katika eneo la Area D mjini hapa wamelalamikia uchafu uliokithiri kwenye majengo hayo.

Wakizungumza leo Jumanne Aprili 24, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka 2018/19, mbunge wa viti maalumu (CCM), Mwanne Nchemba na Joyce Mukya (viti maalumu-Chadema) wamesema uchafu huo umekuwa kero kwao.

Mwanne amesema maghorofa hayo yamezingirwa na uchafu uliokithiri kutokana na wakala huo kushindwa kuyafanyia usafi.

“Nitoe ushauri kwa TBA walete waraka maalumu wa kututaka kuchangia angalau Sh10,000 kwa ajili ya usafi. Wapangaji wana uwezo huo wa kulipa,”amesema.

Amesema kwa sababu kodi wanayotoa ni ndogo wapangaji watoe fedha hizo na TBA watafute kampuni ya kufanya usafi katika mazingira hayo.

Kwa upande wake, Joyce amesema wapangaji wamekuwa wakilipa kodi ya pango ya Sh150,000 na Sh250, 000 kwa nyumba moja, lakini mazingira ya eneo hilo yamegubikwa na uchafu.

“TBA haijawahi kufanya usafi hata wa kupaka rangi katika majengo haya,” amesema.

Amesema ukarabati unaofanyika katika majengo hayo ni kwa ajili ya nyumba za viongozi wanaohamia Dar es Salaam.

.