Wabunge waliotajwa kutekwa waanza kuchukua tahadhari

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (kushoto) akizungumza jambo na mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (katikati) na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe walipohudhuria kikao cha tano cha mkutano wa Bunge la Bajeti mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

NUKUU
“Nadhani ama hofu ya watu au watu wenye nia ya kutengeneza taharuki za kutaka kuchafua nchi yetu. Kwa hiyo mimi kama waziri ninayeshughulikia masuala ya usalama wa raia kwa ujumla ninawaambia hakuna kitu kama hicho.”
Mwigulu

Dodoma. Taarifa ya Mbunge wa  Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kuwa wabunge 11 wamo katika orodha ya watu wanaoweza kutekwa wakati wowote, imesababisha waliotajwa kurekebisha mienendo yao kuepuka kunaswa huku wakisema hawana hofu.

Bashe, ambaye alisema bungeni kuwa alitekwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa kuna wabunge ambao bado wanasakwa na maofisa hao.

Mitandao ya kijamii ilichukua taarifa hiyo na kuiongezea nyama, ikiwataja wabunge hao kuwa ni Bashe, Aeshi Hilaly (Sumbawanga Mjini-CCM), Mwita Waitara (Ukonga-Chadema) na Tundu Lissu (Singida Mashiriki-Chadema).

Wengine ni Mwigulu Nchemba, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini-ACT Wazalendo) na Nape Nnauye, mbunge wa Mtama kwa tiketi ya CCM ambaye alitishiwa bastola na askari kanzu wakati akielekea kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kuvuliwa uwaziri.

Wakizungumza na Mwananchi, wabunge hao walisema tangu kutajwa kuwa wanasakwa, wameanza kuishi kwa tahadhari.

“Nimeanza utaratibu wa kutoa taarifa ya sehemu ninayokwenda,” alisema Bashe.

“Lakini vitisho hivyo haviwezi kubadilisha mfumo wangu wa maisha wala kubadilisha ninachokiamini.”

Bashe alisema alilazimika kulizungumzia suala hilo bungeni kwa kuwa vitisho si dhidi yake pekee, bali wabunge wengine na Watanzania kwa ujumla.

Bashe alisema kwa kuwa Serikali inaongozwa na CCM, jukumu lake na wabunge wenzake ni kuisimamia kwa sababu mkataba ni kati ya wananchi na CCM.

“Chama kinaunda Serikali ambayo ni wakala wa chama kutekeleza mkataba ambao chama kiliingia na wananchi,” alisema Bashe.

 “Naamini jukumu la kuisimamia, kuishauri, kuikosoa na kuilinda Serikali ni jukumu la mbunge wa CCM, zaidi kuliko wa chama kingine. Sasa kinapotokea kitu kinacholeta picha mbaya kwa Serikali ni lazima tusimame na kukipigia kelele.

 “Tukumbuke unapofika uchaguzi, Chama cha Mapinduzi kinaenda kuomba kura na si Serikali. Huko (wabunge) tutahojiwa na wananchi, watatupima tunawasemeaje walikotutuma (bungeni).

“Na siasa ni perception (mtazamo) ikifika Watanzania wakaona ama kuamini kuwa anayewasemea si mbunge wa CCM, bali ni wa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) Ukawa, tutahatarisha uhai wa chama chetu.”

Mbunge mwingine aliyesema ameanzisha utaratibu kama wa Bashe ni Aeshi, ambaye alisema hupiga simu kuwaeleza watu wake wa karibu sehemu anapoenda baada ya kutishiwa uso kwa uso na kiongozi wa Serikali mkoani Dar es Salaam.

“Mwenzako tangu nitishiwe na yule kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, nimekuwa nikiishi kama popo na kila sehemu ninapoenda napiga simu kwa watu mbalimbali kuwaeleza sehemu nilipo. Hata kwenye simu yangu nimetegesha (GPS) kwa ajili ya (wengine) kujua eneo nilipo,” alisema Aeshi.

Lakini Waziri Mwigulu, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), alisema hakuna kitu kama utekaji na kuwataka wabunge wengine kuondoa hofu.

“Ngoja nikwambie, kwanza hakuna kitu kama hicho. Pili hakuna sababu kama hiyo na tatu nchi yetu haijafikia hatua kama hiyo,” alisema Mwigulu.

“Nadhani ama hofu ya watu au watu wenye nia ya kutengeneza taharuki za kutaka kuchafua nchi yetu. Kwa maana hiyo mimi kama waziri ninayeshughulikia masuala ya usalama wa raia kwa ujumla ninawaambia hakuna kitu kama hicho.”

Mwigulu alisema yeye binafsi hana hofu yoyote ya kutekwa na anapenda kuwaambia wabunge wengine waliopata tishio la kutekwa kuwa wasiwe na hofu kwa kuwa jambo hilo halipo.

Mbunge mwingine aliye kwenye orodha hiyo, Zitto, ambaye aliwahi kuamua kutotoka viwanja vya Bunge hadi usiku aliposaidiwa na Spika baada ya kupata taarifa za kukamatwa, alisema kumekuwa na taarifa kama hizo mara nyingi.

 “Mwaka jana niliambiwa kuwa wabunge tunaowindwa tupo watatu, mwanzoni mwa mkutano huu wakawa saba. Wakati huu wa Bunge la Bajeti nikajulishwa kuwa tumefikia saba. Sasa naona idadi iliyotangazwa na Mheshimiwa Bashe inasema ni wabunge kumi na moja wanaotakiwa kutekwa,” alisema Zitto.

“Nadhani ni mambo ya kupeana hofu tu. Kwanza, sijafanya lolote la kusababisha nitekwe, kuteswa na kupotezwa. Hivyo habari hizi nazidharau kwa sababu sioni sababu kwanini nitekwe.”

Zitto, ambaye mapema wiki hii alitoa taarifa ya kutaka kuwasilisha hoja ya kutaka Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza matukio yote ya utekaji na wananchi kuteswa, alisema kama kweli watu wenye mpango wa kumteka wapo, wajipange vizuri na wajiandae sana.

“Wanaweza kupanga kuniteka wakanifuata wakakuta mti wa mrumba au Bwawa la Karosho au Ziwa Tanganyika. Wathubutu tu wataona.” alisema Zitto

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Nape. “Nimeyasikiasikia na kuyasoma kwenye mitandao ya kijamii, ila binafsi siamini na sidhani kama kuna mtu anaweza kuniteka. Hayo ni maneno ya mitaani,” alisema Nape, ambaye alikuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Lakini Waitara, ambaye ni Mbunge wa Ukonga, alisema ameanza kuishi kwa hofu baada ya kupata taarifa kuwa anasakwa ili atekwe.

“Maisha yangu ni ya wasiwasi kwa sababu mtoa taarifa anasema hao watu wanaotaka kutukamata wapo 14. Wameelekezwa waje Dodoma na sehemu wanayotuvizia ni kwenye geti la kutokea bungeni,” alisema Waitara.

Waitara alisema wabunge wenzake hawana ulinzi na  ameiomba Serikali kuchukua hatua kwa sababu mtu aliyempa hiyo taarifa yupo katika mfumo wa Serikali.

“Nimechukua hatua za ulinzi binafsi kwa namna ambayo siwezi kusema ni ulinzi upi, ila kwa sasa nimekuwa mwangalifu na sehemu ninazokwenda kutembelea,” alisema Waitara.

Waitara alisema amekuwa mwangalifu hata kwa simu anazopokea, kwa zile simu za watu ambao hawajui inambidi awaambie watu wake wa karibu kuwa amepigiwa na mtu fulani na anakwenda sehemu fulani kukutana naye.

Mbunge wa Singida Mashariki, Lissu, ambaye ameyaelezea matukio ya kukamatwa kwake na polisi akiwa bungeni na jimboni na kusafirishwa hadi Dar es Salaam bila ya kibali kuwa ni ya utekaji, alichukulia taarifa hizo kwa uzito.

“Matukio ya utekaji na watu kuteswa na wengine wakipotea kabisa yanaendelea kuongezeka katika nchi yetu. Kwa hiyo si jambo la kupuuzia hata kidogo,” alisema Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika .