Wabunge wapigia debe mahitaji ya walemavu

Muktasari:

Watu wenye ulemavu watakiwa kuwa na wawakilishi katika mabaraza ya madiwani

 Wabunge wamesema bado ujenzi wa miundombinu nchini haujazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu hivyo kuwafanya kushindwa kupata huduma nyingine za kijamii.

Walisema hayo jana katika kikao cha mashauriano kilichoshirikisha Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (Shivawata), Shirika la Kimataifa la Add, wajumbe wa kamati tatu za Bunge za Bajeti, Huduma za Maendeleo ya Jamii, Katiba na Sheria.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Mollel alishauri wabunge wa majimbo kutenga asilimia mbili ya fedha za mfuko wa jimbo kugharamia ujenzi wa miundombinu hasa vyoo katika shule kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dalaly Kafumu alishauri watu wenye ulemavu kuwa na wawakilishi katika mabaraza ya madiwani nchini ili waweze kuwasemea.

“Katika ngazi ya Bunge, tunauwakilishi lakini kuna umuhimu sasa wa kuwa na wawakilishi hadi ngazi ya chini ya uongozi ya halmashauri ambako ndiko kuna watu wenye ulemavu wengi,” alisema.

Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago alisema haungi mkono wazo la kuanzishwa kwa benki ya watu wenye ulemavu kama watu wengine wanavyotaka kwa sababu itachangia unyanyapaa.

“Mimi siungi mkono wazo la kuanzisha benki maalumu kwa watu wenye ulemavu, isipokuwa tuwahamasishe wenye mabenki kujenga miundombinu ambayo hata mtu mlemavu anayetumia ‘wheel chair’ anaweza kupata huduma ATMs,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Jitu Soni alisema vifaa vingi vya watu wenye ulemavu bado vinalipishwa kodi, hivyo kuchangia watu wanaojitolea kuviagiza kushindwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Maendeleo ya Huduma za Jamii, Juma Nkamia alisema suala la misamaha ya kodi linahitaji uaminifu mkubwa ili kuwaepuka watu wanaotumia mianya hiyo kukwepa kodi.

Meneja Programu wa Add, Isack Mdama alisema kwamba shirika hilo limejenga vyoo vinne vya mfano vinavyoweza kujengwa katika shule nchini ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na faragha.

“Tumejenga vyoo vinne vinaweza kujengwa katika shule mbalimbali na kuwapa faragha walemavu wanaotumia wheel chair. Choo kikijengwa kwa mfumo unaomwezesha kwenda mwenyewe kinampa faragha zaidi (mwenye ulemavu) ambayo mimi na wewe tunaitaka.”