Wabunge wataka mahindi yaliyohifadhiwa yauzwe

Muktasari:

Uamuazi huo umetolewa na wabunge wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na uhaba wa chakula.

Wabunge wameitaka Serikali kuwauzia wananchi chakula kilichohifadhiwa kwenye ghala mkoani Shinyanga.

Uamuazi huo umetolewa na wabunge wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na uhaba wa chakula.

Wajumbe wa kamati hiyo wameamua hivyo baada ya ziara katika ghala la chakula lililopo Shinyanga ili kuona kama bajeti ya Serikali imetumika na kukuta likiwa na tani 8,622 za mahindi zilizohifadhiwa. Kutokana na hatua hiyo, wameagiza chakula hicho kiuzwe kwa wananchi kwa bei nafuu ili kisiharibike.

Wabunge hao wamesema inasikitisha kuona mahindi yanahifadhiwa ndani ya miaka mitatu huku wananchi wakiendelea kulia njaa na kununua chakula kwa bei ya juu.

Mjumbe wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini amesema NFRA haina budi kuangalia sehemu zenye uhitaji wa chakula na kuwauzia wananchi chakula hicho.

“Ushauri wetu ni kuwaomba mfanye utaratibu muuze mahindi haya hata kwa Sh20,000 kwa debe moja ili kukiokoa chakula hiki na kupunguza malalamiko ya njaa kwenye jamii,” amesema mbunge huyo.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Deusdedit Mpanzi amesema hadi kufikia Machi 20, mwaka huu wameshanunua tani 62,099.319 na kati ya hizo tani 38,162.280 sawa na asilimia 61.5 zimenunuliwa katika vituo vya ununuzi, na tani 23,937. 03 sawa na asilimia 38.5 zimenunuliwa kwenye vikundi vya wakulima.