Wabunge wataka uchunguzi ugawaji vitalu vya uwindaji

Muktasari:

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo jana, makamu mwenyekiti wake, Kemilembe Lwota alisema walikutana na wadau wa uwindaji wa kitalii na kupokea malalamiko kuhusu hatua ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kufuta leseni zote za umiliki wa vitalu kwa kipindi cha mwaka 2018/2022 zilizotolewa kihalali na wizara.

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeliomba Bunge kuazimia kuunda kamati ndogo ya uchunguzi kujiridhisha na hatua ya Serikali ya kugawa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada na uboreshaji mwingine.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo jana, makamu mwenyekiti wake, Kemilembe Lwota alisema walikutana na wadau wa uwindaji wa kitalii na kupokea malalamiko kuhusu hatua ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kufuta leseni zote za umiliki wa vitalu kwa kipindi cha mwaka 2018/2022 zilizotolewa kihalali na wizara.

Alisema Serikali inapaswa kufahamu kuwa biashara ya utalii inahitaji umakini, hivyo mabadiliko kidogo yanaweza kuathiri mpango mzima.

Kemilembe alisema biashara hiyo inahitaji muda kujipanga, kuitangaza na kuwapa imani watalii na wawekezaji katika sekta hiyo.

Alisema watalii wa uwindaji wamesitisha safari mara nyingi kutokana na kukosekana kwa uhakika wa biashara hiyo.

Alisema mwenendo wa mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii unaonyesha mapato ya uwindaji wa kitalii yameshuka kutoka dola milioni 23.5 mwaka 2010 hadi kufikia dola milioni 11.2 kwa mwaka 2015.

Pia, alisema kamati inalishauri Bunge liunde kamati teule kuchunguza malalamiko na migogoro kati ya wahifadhi na wafugaji ili iweze kubaini na kushauri Serikali hatua za kuchukua kumaliza malalamiko ya migogoro hiyo.

Kemilembe alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya wafugaji kuhusu kukamatwa mifugo yao kwa madai kuwa wameingiza katika hifadhi.

Alisema migogoro hiyo imesababisha uhasama, rushwa na mifugo kupigwa mnada au kutaifishwa kinyume cha sheria.

Kuhusu ujangili

Kamilembe alisema kamati ilitaarifiwa uwepo wa mbinu mpya ya ujangili ambapo majangili wanatumia sumu kuua wanyamapori.

Alisema mbinu hiyo mpya ni hatari kwa uhifadhi si tu inaua wanyama wengi kwa wakati mmoja bali pia inaua wanyama wasiokusudiwa.

Alisema pia majangili wamekuwa wakibadili mbinu za usafirishaji nyara za Taifa mara kwa mara na kufanya udhibiti kuwa mgumu.

“Kamati inaishauri serikali kubadili mbinu za kupambana na majangili kwa kuongeza vifaa vya mawasiliano, silaha za kisasa na kuunda kikosi maalumu kupambana na ujangili. Pia, kutumia kikosi cha intelijensia kubaini mtandao wa ujangili wa tembo ili kuokoa rasilimali muhimu iliyo hatarini kutoweka,” alisema.

Kamati imeipongeza Serikali kwa kuanzisha utaratibu wa kuwa na jeshi Usu kulinda rasilimali za wanyamapori.

Serikali imeshauri pia kufanya uchunguzi ili kujua boti zinazotia nanga usiku katika Hifadhi ya Taifa ya Saadan zinafika kufanya nini na zinabeba vitu gani.

Mwisho.