Wabunge wenye vichanga sasa kunyonyesha bungeni

Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Sharon Sauwa akiwa kwenye chumba maalum kitakachotumika kwa ajili ya wabunge kunyonyeshea watoto wao kilichopo kwenye ukumbi wa  Pius Msekwa uliopo eneo la Bunge mjini Dodoma. Picha na Emmanuel Herman

Muktasari:

  • Wabunge wanaonyonyesha watoto wadogo, sasa hawatakuwa na mawazo ya kufikiria kurudi majumbani au hotelini kutimiza wajibu huo, badala yake wanasogezewa huduma hiyo karibu.
  • Ofisi ya Bunge imetenga chumba maalumu cha kunyonyesha, jambo ambalo litakuwa faraja kubwa kwa wabunge wanaonyonyesha.

Dodoma. Mambo yamezidi kunoga katika Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini hapa, na sasa mambo yanakwenda kisasa zaidi.

Wabunge wanaonyonyesha watoto wadogo, sasa hawatakuwa na mawazo ya kufikiria kurudi majumbani au hotelini kutimiza wajibu huo, badala yake wanasogezewa huduma hiyo karibu.

Ofisi ya Bunge imetenga chumba maalumu cha kunyonyesha, jambo ambalo litakuwa faraja kubwa kwa wabunge wanaonyonyesha.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu jana asubuhi, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alitangaza uamuzi huo, akisema chumba hicho kitakuwa karibu na ofisi ya ulinzi katika jengo la Msekwa ambalo awali lilikuwa likitumika kwa vikao vya chombo hicho.

“Ofisi ya Bunge inawataarifu kuwa imetenga chumba maalumu kwa ajili ya kunyonyeshea kwa wabunge walio na watoto wachanga,” alisema Dk Tulia.

Aliwasihi wabunge wenye watoto wachanga kuwanyonyesha angalau kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee.

Hatua hiyo imepongezwa na wabunge wengi hasa wenye watoto wanaonyonya, ambao hata hivyo baada ya kukikagua chumba hicho, wameshauri kiboreshwe.

Wametaka kiboreshwe kwa kuwekewa kitanda, maji ya moto na vitu vya kuchezea watoto.

Jana, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alitangaza kuwa Ofisi ya Bunge imetenga chumba maalumu kwa ajili ya wabunge kunyonyesha wakati vikao vikiendelea.

Alisema chumba hicho kiko ukumbi wa Pius Msekwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Bunge jana, baadhi ya wabunge wanawake walipongeza hatua hiyo ya kutenga chumba maalumu kwa ajili ya kunyonyesha.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Felister Bura alisema uamuzi huo ni mzuri kwa sababu utawapunguzia muda wabunge hao kwenda nyumbani kwa ajili ya kunyonyesha.

“Mimi naona ni hatua nzuri kwa sababu sasa wanaweza kunyonyesha, kuendelea na vikao vya bunge na pia wanaweza kupata huduma za zahanati kama kuna tatizo limejitokeza,” alisema.

Mbunge wa viti maalum (Chadema), Tunza Malapo alipongeza hatua hiyo lakini akataka hatua inayofuata iwe ni kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya watoto hao wanapokuwa eneo hilo.

Alisema kama ni chumba kwa ajili ya watoto wachanga na waangalizi kuwepo wakati wote mbunge anapoendelea na majukumu yake kinatakiwa kiwe na huduma mbalimbali.

“Inategemea. Je, wanakuja tu na kuondoka baada ya kunyonyeshwa? Ama wanakaa kwa kipindi chote wakati tunaendelea na majukumu yetu? Kama ni wakati wote, je, mazingira ya chumba yakoje?” alihoji mbunge huyo mwenye mtoto wa miezi sita.

“Je, kuna kitanda ambacho unaweza kukitumia kwa ajili ya kumbadilisha mtoto nguo anapojisaidia? Kuna maji ya moto kwa ajili ya kumsafishia kwa sababu ya baridi ya huku?”

Mbunge mwingine ambaye ana mtoto wa miezi minane, Yosefa Komba (Chadema) alishauri chumba hicho kiwekewe mazingira ambayo yatawezesha watoto hao kukaa kwa furaha bila bughudha wakati wa vikao.

“Mazingira wezeshi ni jambo muhimu katika chumba hicho. Licha ya vitanda, kuna michezo ya watoto ama ni kwa ajili ya kunyonyesha tu na mtoto kuondoka?” alihoji.

Nje ya ukumbi wa Bunge, Dk Tulia alisema wabunge wataruhusiwa kuja na wasaidizi kwa ajili ya uangalizi wa watoto wakati vikao vikiendelea.