Wachambua adhabu waliyopewa Komu, Kubenea Chadema

Muktasari:

Ni kufuatia uamuzi wao kukiri hadharani kuwa walitaka kumdhuru Meya wa Ubungo, Boniface Jacob

Dar es Salaam. Siku moja baada ya wabunge wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Antony Komu (Moshi Vijijini), kuomba radhi hadharani baada ya kukiri sauti iliyosambaa kwenye mitandao ya jamii ikiwahusisha watu wawili wanaopanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kuwa ni yao, wameibua maoni tofauti kutoka kwa wadau wa siasa.

Juzi, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alitangaza maazimio yaliyofikiwa na kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichoketi kujadili sakata hilo ambalo pamoja na mambo mengine, wabunge hao walitakiwa kuomba radhi hadharani.

Licha ya kuomba radhi, pia walipewa onyo wakitakiwa kuandika barua za kuwaomba radhi waliotajwa kwenye mazungumzo hayo, wamevuliwa nafasi za uongozi ndani ya chama na kubakiwa na ubunge pamoja na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa miezi 12. Kulingana na maoni ya wadau, hatua hiyo imetafsiriwa katika pande mbili; mosi ikiwa ni pongezi kwa uamuzi uliochukuliwa huku upande mwingine ukikosoa utaratibu huo na kueleza kuwa msamaha ulioombwa na wabunge hao haukuwa wa dhati.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana alisema hatua waliyochukua wabunge hao ni ya kiungwana na inayoonyesha ukomavu kwa kukubali kuomba radhi hadharani.

Hata hivyo, alisema hadi sasa hafahamu sababu hasa ya wabunge hao kuomba radhi kama walichokizungumza ndicho kilikuwa ndani ya mioyo yao.

Profesa Bana alisema ana imani kuwa kitendo cha wabunge hao kutoka hadharani na kuomba radhi kimetokana na msukumo walioupata ndani ya chama, lakini siyo kwa ridhaa yao. “Hawa wamelazimishwa kuomba radhi kwa kuwa wameona kuwafukuza itawagharimu, hivyo wakaona ni bora waombe radhi,” alisema.

Alisema licha ya uamuzi wa chama kuwataka waombe radhi, haina maana kuwa itawaondolea dhamira iliyowasukuma kuzungumza maneno yaliyosikika.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kilichofanywa na Chadema na wabunge hao ni ulaghai.

Alisema Kubenea na Komu hawakuonekana kwamba nafsi zao zimeamua kuomba radhi, bali walifikia uamuzi huo baada ya kulazimishwa.

“Wale walishurutishwa ndiyo maana hata hawaonekani kuwa wanaomba msamaha kwa dhati, bado wana dukuduku, walichozungumza si kigeni kila siku kinasemwa, kukubali kuomba radhi ni unafiki,” alisema.

Kuhusu Chadema, Muabhi alisema imeamua kutowafukuza wabunge hao kutokana na kulinda masilahi ya chama.

Hata hivyo, alisema uamuzi uliofikiwa unaweza kuonekana mzuri, lakini ni hatari kwa ustawi wa chama kwa kuwa utendaji wa wabunge hao ndani ya Bunge hauwezi kuwa kama ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake, Dk Richard Mbunda wa UDSM alisema anaamini uamuzi wa Komu na Kubenea ulitoka ndani ya nafsi zao.

“Sidhani kama walilazimishwa, wana haki na uwezo wa kukataa. Kitendo cha kutoka mbele ya hadhira na kuomba radhi kimeonyesha wana imani na chama chao na wanataka kuendelea kuwa humo,” alisema.

Dk Mbunda alisema sakata hilo lilikuwa kipimo cha uvumilivu na busara kwa viongozi wa Chadema katika kushughulikia matatizo yao ndani.

Mwananchi lilimtafuta Kubenea ambaye alishangazwa na maneno kwamba hakuonyesha umakini (serious) wakati wa kuomba msamaha, ambapo alijibu kwa kifupi, “Usiriazi wa mtu unaupimaje, kwa ninavyofahamu hilo liko moyoni mwa mtu. Wangapi wana maneno mengi lakini vitendo hakuna na wangapi wapo kimya halafu matendo yao yanaonekana.” Kuhusu kuvaa miwani iliyoficha macho yake, Kubenea alisema aliivaa kwa sababu ya tatizo lake la macho na si vinginevyo.

“Miwani ile nilipewa na daktari India kwa sababu ya tatizo langu la macho, imetengenezwa mipana vile ili kuzuia upepo na vumbi na rangi yake nyeusi inayakinga na jua. Daktari amenishauri niwe navaa mara kwa mara, hii siyo miwani ya mitaani.”