Wachimbaji: Dhahabu itumike kama dhamana benki

Muktasari:

Wachimbaji wa dhahabu wameshauri taasisi za fedha kuwa na utaratibu wa kutumia dhahabu kama dhamana badala ya kutegemea dhamana nyingine kama mashamba na nyumba

Geita. Baadhi ya  wachimbaji wa dhahabu mkoani Geita wamezishauri taasisi za fedha nchini kuweka kitengo cha kutunza dhahabu kama dhamana badala ya kutegemea dhamana za mashamba na nyumba pekee.

Imeelezwa kuwepo kwa kitengo hicho kutawawezesha wachimbaji kuendelea kuchimba kwa faida hasa wakati ambao bei ya dhahabu katika soko la dunia itakua imeshuka.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Septemba 26, 2018 mmoja wa wachimbaji wadogo, Godfrey Miti amesema taasisi za fedha zikikubali dhahabu kuwa dhamana na kuzitunza itamuwezesha mchimbaji kukopa na kuingia kwenye uchimbaji wa kisasa ambao una tija.

“Soko la dhahabu halitabiriki lakini kama benki zitakubali kuhifadhi dhahabu kama dhamana na mchimbaji akaendelea kuchimba ni wazi bei ikipanda mchimbaji atanufaika lakini pia Serikali itapata kodi kubwa tofauti na bei ya soko ikiwa ndogo,” amesema.

Sia Hussein, mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wanawake mkoani hapa ameiomba Serikali kutafuta mbadala wa zebaki kutokana na kemikali hiyo kuwa na madhara makubwa kwa wachimbaji.

Amesema kina mama wengi wanaotumia kemikali ya zebaki kunasa dhahabu wamekuwa wakipata madhara mengi ya kiafya ikiwemo kuchubuka mikono na baadaye kupata saratani.