Friday, May 19, 2017

Wachimbaji wawili wafia ndani ya mgodiPicha/Maktaba

Picha/Maktaba 

By Hakimu Mwafongo, Mwananchi hmwafongo@mwananchi.co.tz

Iringa. Wachimbaji wawili wa madini katika kijiji cha Masuluti mkoani hapa, Haus Kaijage (32) mkazi wa Bukoba na James Mlawa(22) mkazi wa Magulilwa, Iringa wamefariki dunia baada ya kukosa hewa ndani ya mgodi.

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Masuluti, Venjaslaus Kiunosile amesema tukio hilo limetokea leo (Ijumaa) saa tano asubuhi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa, Julius Mjengi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari miili ya marehemu imetolewa ndani ya mgodi.

Amesema chanzo cha watu hao kupoteza maisha ni kukosa hewa baada ya kuingiza jenereta la kuvuta maji mgodini kwa lengo la kuvuta maji na baada ya kuliwasha walikosa hewa.

Hata hivyo amesema jeshi la polisi linamshikilia mmiliki wa mgodi huo Samweli Msigwa kwa mahojiano

 Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Mgama, Baraka Mwifune amesema uchunguzi wa awali uliofanywa umeonyesha kuwa watu hao walipoteza maisha kwa kukosa hewa.

Mmiliki wa mgodi huo, Msigwa amesema  akiwa njiani kuelekea eneo la mgodi kwa ajili ya kusaidia kutengeneza mashine ya kuingiza hewa katika mgodi huo ndipo alipopata taarifa ya wachimbaji hao wawili kati ya sita kupoteza maisha kwa kukosa hewa.

-->