Wednesday, September 13, 2017

Wachina wakamatwa Dodoma wakiwa na kucha za Simba

By Ben Patrick, Mwananchi

Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia raia watano wa China kwa tuhuma za kumiliki nyara mbalimbali za Serikali kinyume na sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema Septemba 11 mwaka huu raia hao walikamatwa katika Kijiji cha Mpamatwa, Wilaya ya Bahi mkoani hapa wakiwa na na kucha nne za simba.

Amesema pia wamekamatwa jino moja la simba, magamba 652 ya mnyama kakakuona pamoja na kucha zake tano.

“Upepelezi bado unaendelea kujua mtandao wa majangili wageni wanaoingia nchini na kujihusisha na uhalifu,” amesema Kamanda Muroto.

Pamoja na hilo Kamanda Muroto amesema jeshi la polisi mkoani Dodoma linaendelea na msako wa kuwasaka wahalifu mbalimbali na wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 12 wa uvunjaji na wizi.

Watuhumiwa hao pia wamekamatwa na vifaa mbalimbali vya nyumbani ikiwemo televisheni 13 na radio mbili.

Pia mmoja wa watuhumiwa hao aliyetambulika kwa jina la Dotto Kapenga alikamatwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Zikiwa na cheo cha Luteni Ussu.

-->