Wachoma moto lori lililomgonga mwendesha bodaboda, kuua abiria

Muktasari:

Kamanda awataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi

 Wananchi wenye hasira wameliteketeza kwa moto lori lililomgonga mwendesha pikipiki na kusababisha kifo cha abiria wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema tukio hilo lilitokea eneo la Kaseme mjini Geita Machi 13.

Alimtaja aliyepoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni muuguzi wa Zahanati ya Kaseme, Martha Paulo (30).

Kamanda Mwabulambo alisema baada ya ajali hiyo, wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa kuliteketeza kwa moto lori lililohusika kwenye ajali hiyo.

Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa bodaboda aliyekuwa akiyapita magari yaliyokuwa mbele yake kwenye eneo lenye muinuko bila kuchukua tahadhari.

“Mwendesha pikipiki alikuwa akijaribu kulivuka lori lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na kukutana uso kwa uso na lori lingine; alipojaribu kurudi upande mwingine akajigonga kwenye lori alilokuwa akijaribu kulivuka na kusababisha kifo cha abiria wake pale pale,” alisema Kamanda Mwabulambo.

Aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi na kuonya kuwa jeshi hilo litawachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mayala Bishibe alisema pamoja na uzembe wa mwendesha pikipiki, utelezi uliokuwapo barabarani kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha pia ulichangia ajali hiyo.

Alisema wakati ajali hiyo inatokea, abiria alikuwa amewabeba watoto wawili ambao hawajapata majeraha yoyote.

Mkazi mwingine wa eneo la Kasema, Fanuel Gispson alihusisha ajali hiyo na ufinyu wa barabara katika eneo la ajali anayosema ilimfanya mwendesha pikipiki kushindwa kuyakwepa malori hayo.