Wachumi washtushwa na kasi ya kufungwa biashara Dar, Arusha

Muktasari:

Juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali imebaini kuwa karibu wafanyabiashara 2,000 wamefunga biashara zao Dar es Salaam na Arusha lakini akasema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia saba na unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka huu.

Dar es Salaam. Wataalamu na wadau wa uchumi na biashara wameeleza kushtushwa na taarifa za wafanyabiashara kufunga biashara zao na kushuka kwa ukuaji wa kilimo, huku wakiitaka Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kusisimua uchumi.

Juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali imebaini kuwa karibu wafanyabiashara 2,000 wamefunga biashara zao Dar es Salaam na Arusha lakini akasema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia saba na unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka huu.

Pamoja na ukuaji huo, Waziri Mpango alisema kilimo kimeshuka kutoka asilimia 2.7 mwaka 2015 hadi asilimia 0.3 mwaka 2016.

Wataalamu wa uchumi na kilimo waliopigiwa simu na mwandishi wetu kuhusu taarifa hiyo ya Waziri Mpango aliyoitoa alipokuwa akizungumzia hali ya uchumi wa Taifa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, walisema hiyo ni ishara mbaya na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja alisema taarifa ya wafanyabiashara kufunga biashara zao inatokana na kilio chao cha muda mrefu kisichosikilizwa na Serikali.

“Tunachokijua ni kuwapo kwa mtikisiko wa uchumi kwa mwaka 2016 kiasi kwamba wafanyabiashara wanalalamika kukosa wateja. Siyo kufunga biashara tu, wengine wamerudisha hata TIN (namba ya utambulisho wa mlipakodi) kwa kushindwa masharti,” alisema Minja. “Tunachotofautiana na Serikali ni kuhusu sababu, sisi tunachojua chanzo ni masharti magumu ya kufanya biashara ndicho kinachowashinda watu. Sasa kama Waziri Mpango hajui basi kuna udhaifu kiuongozi.”

Alikuwa akizungumzia kauli ya waziri kwamba sababu za kufungwa kwa biashara hizo hazijabainika kutokana na ugumu wa kupata taarifa kwa wahusika, lakini akabainisha sababu tano za jumla zinazoweza kuwa chanzo ambazo alizitaja kuwa ni kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au kulipwa madeni, kubadilisha aina ya biashara, kushindwa kusimamia biashara, gharama kubwa za uendeshaji na wabia katika biashara kutoelewana.

Minja aliitaka Serikali kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara: “Unapoona mlipakodi mmoja kati ya 99 anajitoa, unatakiwa uwaache hao 99 umrudishe huyo mmoja, lakini kama hujui hata sababu, basi huo upungufu kiuongozi,” alisema Minja.

Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema kushuka kwa ukuaji wa kilimo kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 0.3 ni ishara kuwa umaskini umeongezeka.

“Ni wazi kwamba katika mwaka mmoja, tumetengeneza maskini wengi kuliko miaka mingine iliyopita. Tusijidanganye kwamba kuna sekta nyingine kama madini au gesi ndivyo vitabeba uchumi wetu. Hata uchumi wa viwanda unategemea kilimo,” alisema Rukonge.

Akizungumzia hali ya kilimo na biashara, Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Sokoine, Ntengua Mdoe alisema imekuwa mbaya kwa sababu Serikali haiwekezi.

“Wananchi wengi wanategemea kilimo, japo kuna baadhi ya sekta zinazokuza uchumi. Kama ukuaji wa kilimo umeshuka, basi kuna asilimia 75 ya Watanzania wanaendelea kuwa maskini,” alisema.

Profesa Mdoe aliongeza, “Hata biashara zimekuwa ngumu, tunaona hoteli zikifungwa hapo Dar es Salaam na nyingine zikibadilishwa matumizi, ni kwa sababu hakuna mzunguko wa fedha, uwezo wa watu kununua umeshuka. “Serikali inapaswa kuongeza fedha kwenye mzunguko hasa kwenye sekta binafsi ili uwezo wa kununua uongezeke.”

Mtaalamu aliyebobea katika uchumi, Profesa Samuel Wangwe alisema ukuaji wa uchumi hautakuwa endelevu kama kilimo hakikui.

“Kama hali ya hewa itakuwa nzuri basi na uchumi nao utakuwa mzuri, lakini hali ikiwa mbaya na mavuno yasipopatikana, uchumi hauwezi kukua.”

Profesa Wangwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ameishauri Serikali kujenga uhusiano na sekta binafsi ili iweze kuajiri na kulipa kodi.