Wadau wa mkonge wakerwa na matumizi ya mazulia ya plastiki serikalini

Muktasari:

  • Wamesema matumizi ya bidhaa za mkonge badala ya plastiki pia yatasaidia kutunza mazingira ambayo kila siku yamekuwa yakiharibika ikiwamo ardhi kushindwa kuotesha mazao.

Tanga. Wadau wa mkonge nchini wamemuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kulifikisha kwa Rais John Magufuli ombi lao la kutaka ofisi za Serikali ziagizwe kutumia mazuria na kamba za mkonge badala ya plasitiki ili kukuza viwanda vya ndani ya nchi.

Wamesema matumizi ya bidhaa za mkonge badala ya plastiki pia yatasaidia kutunza mazingira ambayo kila siku yamekuwa yakiharibika ikiwamo ardhi kushindwa kuotesha mazao.

Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi, Agosti 17 na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte wakati wa mkutano wa jukwaa la fursa za biashara Mkoa wa Tanga lililofunguliwa na Waziri Mwakyembe na kuandaliwaa na Tanzania Standard News Paper (TSN).

Amesema licha ya kuwa kiwanda kikubwa kuliko vyote barani Afrika cha kutengeneza bidhaa mbalimbali za mkonge, matumizi ya bidhaa zitokanazo na plastiki yanazidi kushamiri nchini.

Mkurugeniz huyo amesema hata kwenye taasisi za Serikali mazuria yanayotumika ni ya kutoka nchi za nje na ya plastiki.

"Kila mmoja hapa anafahamu jinsi Rais wetu alivyo…kama atatoa agizo kwamba kuazia leo sitaki kuona ofisi yoyote ya Serikali isiyotumia mazuria ya mkonge na akitishia kuwatumbua wahusika basi sekta ya mkonge nchini itakuwa kwa kasi,” amesema.

Amesema  ikiwa ofisi zote za Serikali nchini zitaamua kutumia mazuria na bidhaa za mkonge basi ndani ya kipindi kifupi vitajengwa viwanda vingine vitano vya kuzalisha bidhaa za mkonge.

Akizungumza wakati akifungua jukwaa hilo, Waziri Mwakyembe amewataka wakazi wa Tanga kutumia ipasavyo fursa zinazokuja likiwamo bomba la mafuta kwa kuzalisha bidhaa zitakazotumiwaa na wageni.

"Nitashangaa nikisikia wataalamu wa bomba la mafuta wanalala Mombasa au Dar es Salaam na kuja huku kufanya kazi badala ya kulala huku...nitashangaa nikisikia wageni wanakwenda Masaimara kuona vivutio vya utalii badala ya Serengeti au Ngorongoro...nitashangaaa nikisikia wanakodi ndege nje wakati Dar es salaam zipo," amesema Waziri Mwakyembe.

 

Katika jukwaa hilo mashirika mbalimbali ikiwamo Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na

Kilimo (TCCIA) wamewasilisha namna yalivyojipanga kutumia fursa za bomba

la mafuta.