Wadau wawanyooshea vidole wanaowapa mimba watoto wa kike

Muktasari:

  • Wadau hao walitolea mfano ng’ombe wakisema hawezi kumzalisha ndama.
  • Hayo yameelezwa jana wakati wa mjadala wa kumuinua mwanamke uliofanywa na Taasisi ya Jinsia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na ubalozi wa Marekani.

Dar es Salaam. Wanaume wanaowapa mimba watoto wa kike wamenyooshewa kidole huku wakielezwa kuwa utashi wao ni mdogo kuliko wa wanyama.

Wadau hao walitolea mfano ng’ombe wakisema hawezi kumzalisha ndama.

Hayo yameelezwa jana wakati wa mjadala wa kumuinua mwanamke uliofanywa na Taasisi ya Jinsia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na ubalozi wa Marekani.

Mjadala huo ulikuwa ni maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa leo. Wanawake wa kada mbalimbali wakiwamo wajasiriamali, wahadhiri, watumishi wa umma na kampuni binafsi pamoja na wanaharakati wa masuala ya jinsia walikutana katika mjadala huo.

Wanawake hao walijadili mbinu za kumnusuru mtoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni.

Akichangia hoja juu ya suala hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Under the Same Sun, Vicky Ntetema alisema wanaume wanaowapa mimba watoto wanaifedhehesha jamii ya Kitanzania kwa kuwa hata wanyama hawafanyi hivyo.

“Swali ni hili, nani anayempa mimba msichana? inawezekana vipi sisi binadamu maarifa yetu yakawa madogo kuliko wanyama? Kwa sababu huwezi kuona ng’ombe akampanda ndama,” alisema.

Alifafanua kuwa elimu inahitajika kwa wanaume ili waachane na tamaa dhidi ya wasichana walio chini ya miaka 18 kwani kufanya hivyo kuna athari nyingi ikiwamo kuwarudisha nyuma kielimu.

Pia, alisema Sheria ya Ndoa inayotumika sasa haitoi ulinzi wa kutosha kwa mtoto wa kike kwa kuwa inaruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 kuozeshwa endapo wazazi wataridhia.

Alishauri elimu ya watu wazima irudishwe ili kutoa nafasi kwa msichana atakayepata mimba akiwa shuleni kuendelea na masomo katika mfumo usio rasmi.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sero Lease and Fiance Limited (SELFINA), Dk Victoria Kisyombe aliyewataka wazazi kusimamia suala la malezi kwa watoto.

Alisema utoaji wa elimu kwa wasichana na wanawake kwa jumla utawawezesha kupambana na changamoto zinazowakabili ikiwamo ukosefu wa mitaji.

“Sheria za nchi ni nzuri, lakini zinakandamizwa na mila kwenye. Wanawake wengi wanashindwa kumiliki ardhi ambayo ingewasaidia kupata mikopo kwenye Taasisi za fedha,” alisema.

Akifungua mjadala huo, Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson alisema jamii imekuwa na tabia ya kusahau baadhi ya makundi wakiwamo wanawake kwenye mikakati ya maendeleo suala ambalo ni kikwazo katika ukuaji wa uchumi.

“Hakutakuwa na jamii huru kama baadhi ya watu hawako huru. Ni lazima tuhakikishe kunakuwa na uhuru wa kijinsia hasa usawa katika umiliki wa ardhi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi,”alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Jinsia cha UDSM, Dk Eugenia Kafanabo alisema msisitizo mkubwa umeendelea kuwekwa katika sekta ya elimu kwa wanawake ikiwa ni njia ya ukombozi wa kijinsia.