Tuesday, February 13, 2018

Wadau wazungumzia tamko la maaskofu Katoliki

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) umeendelea kupongezwa na watu wa kada mbalimbali.

Mwishoni mwa wiki, TEC ilitoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 inayoanza kesho wakizungumzia masuala kadhaa yakiwamo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Miongoni mwa mambo hayo ni uamuzi wa Serikali kuzuia maandamano, mikutano ya hadhara, makongamano na mijadala ya siasa ikisema kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi.

“Licha ya Katiba kuelekeza mfumo wa demokrasia na sheria kuweka utaratibu wa vyama vya siasa, hazifuatwi,” inaeleza sehemu ya ujumbe huo. “...Shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na sheria za nchi.”

Baraza hilo pia limezungumzia hatua ya Serikali kuvibana vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuvifungia kwa sababu mbalimbali na kuingiliwa kwa Bunge na Mahakama likisema hatua hiyo itajenga chuki kiasi cha kuhatarisha amani ya nchi.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ujumbe huo wa TEC, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema, “Tumeuona ila hatuna jibu. Ninachoweza kusema tunawatakia Wakristo wote wa Tanzania na duniani Kwaresima njema.”

Akitoa maoni yake kuhusu ujumbe huo alipotakiwa kufanya hivyo na mwandishi wetu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Helen Kijo-Bisimba alisema, “Tumeupokea kwa kuwapongeza... wanachokizungumza naona walikuwa wanakitafakari kwanza, wamekiona na kukisema.

“Wanakwenda Kwaresima kipindi cha toba, wameona waseme ukweli na watu wanahitaji kutubu na nchi yetu inahitaji toba, kunyimwa uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na mengine,” alisema.

Dk Kijo -Bisimba alitoa wito kwa Serikali akisema, “Irudi katika mstari, bahati nzuri maaskofu hawajasema tubadili sheria, kikubwa ni kurudi katika mstari. Suala la mikutano, kukusanyika na Bunge live hayahitaji kubadili sheria, kwa hiyo Serikali warudi katika mstari.”

Mwingine aliyetoa maoni yake ni Tundu Lissu, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) akisema, “Nimeuona na kuusoma, ninachoweza kusema ni kuwa kwa mara ya kwanza, Baraza la Maaskofu limezungumza kwa umakini sana tofauti na huko nyuma.

“Ni tamko la maana sana ambalo linathibitisha kile ambacho tumekuwa tukikipigia kelele ... uhuru wa kujieleza na mengine. Serikali sasa inapaswa kuufanyia kazi,” alisema Lissu, ambaye yupo Ubelgiji kwa matibabu.

Chama cha ACT-Wazalendo pia kimesema ujumbe wa maaskofu hao unaonyesha jinsi demokrasia inavyominywa nchini. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa chama hicho, Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari jana alisema, “Tunawapongeza sana viongozi wetu wa dini kwa kujitokeza waziwazi kuonyesha hali inaoendelea nchini, “TEC kutoa waraka wa kiuchungaji ni ukurasa mpya katika siasa zetu tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 umalizike,” alisema.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Bakari Kiango, Allence Juma na Mwafatma Hamis.


-->