Waendesha baiskeli kuzunguka Mlima Kilimanjaro kwa siku saba

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Tanzania  Dk Florence Temu akiwa na Katibu mkuu wizara ya habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Suzan Mlawi wakizindua safari ya waendesha baiskeli kutoka nchini Uholanzi ambao wanatarajia kusafari kilimita 400 kuzunguka Mlima Kilimanjaro katika kampeni ya kuchanga fedha kwa ajili ya miradi ya shirika la AMREF. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Lengo kuu ni kuchangia miradi ya kijamii ambayo inaleta maendeleo ikiwamo miradi ya Afya na Elimu nchini

Arusha. Waendesha baiskeli 95 kutoka Uholanzi wameanza  safari ya kilomita takriban 400 itakayochukua siku saba kuuzunguka Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya uchangiaji fedha kwa ajili ya miradi ya Shirika la  Utafiti wa Tiba na Afya Afrika (Amref) ambapo tayari zaidi Sh 1.2 bilioni zimechangwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari ya waendesha baiskeli hao  kupitia kampeni yao ya Africa Classic, iliyofanyika  hoteli ya KIA, katibu mkuu wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na  Michezo, Suzan Mlawi, alisema uchangiaji wa waendesha baiskeli hao una manufaa makubwa kwa taifa.

Alisema licha ya fedha wanazotoa kuchangia sekta ya afya na elimu, lakini pia ujio wao ni kukuza utalii na michezo kwani wengi wao watajifunza mambo mengi na hivyo kusaidia kuvutia watalii kuja Tanzania.

Awali Mkurugenzi Mkazi Amref Tanzania, Dk Florence Temu amesema fedha ambazo wanachanga waendesha baiskeli hao  zinasaidia miradi kadhaa ya Amref ambapo kwa hapa nchini zimesaidia zaidi ya watoto 300,000 katika masuala ya afya ya uzazi na elimu.

Amesema waendesha baiskeli hao, kila mmoja amechanga kwa kiwango cha Euro 5,000 kusaidia miradi ya Amref na katika awamu ya kwanza walikuwa 95 na awamu ya pili watakuja nchini zaidi ya 63.

"Tanzania tumefaidika na fedha hizi kwani tuna miradi ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike na walio katika mazingira magumu na kukosa fursa ya elimu lakini pia fedha hizi zinasaidia kutoa elimu ya kuwakinga watoto katika vitendo vya ukeketaji," amesema.

Kiongozi wa msafara wa waendesha baiskeli hao, Stijn Wopereis kutoka Amref Uholanzi, amesema lengo la kuhamasisha uchangiaji fedha kupitia baiskeli ni kusaidia  kukusanya fedha za kusaidia miradi ya kijamii kwa nchi za Afrika.

"Hawa waendesha baiskeli wamejitolea wenyewe na wanafurahi kuja Tanzania kwa kuwa wanapata fursa pia ya kuona Mlima Kilimanjaro na tamaduni nzuri za kitanzania," amesema.

Mwaka jana, pia walikuja nchini, walichanga zaidi ya Sh1 bilioni kusaidia miradi ya afya na elimu kupitia Amref.