Wafanyabiashara Rukwa watakiwa kujipanga

Muktasari:

Barabara hiyo kutoka mjini Sumbawanga kuelekea wilayani Kalambo hadi Bandari ya Kasanga ina urefu wa km 112 na itafungua fursa ya mawasiliano na nchi jirani hivyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kujiandaa na kuchangamkia fursa hiyo.

Sumbawanga. Wafanyabiashara mkoani Rukwa na maeneo mengine nchini wameshauriwa kuanza kujipanga kufanya biashara nchi za Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wafanyabiashara hao wametakiwa kufanya hivyo mara tu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya Sumbawanga Mjini na kuunganisha na Bandari ya Kasanga iliyopo mkoani Rukwa utakapokamilika.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani aliyasema hayo wakati akiwa katika ziara ya kikazi akikagua ujenzi wa barabara mbalimbali zinazojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa.
Amesema kwa sasa kuna barabara inayojengwa kutoka mjini Sumbawanga kuelekea wilayani Kalambo hadi kwenye bandari ndogo ya Kasanga yenye urefu wa km 112 ambayo itafungua fursa ya mawasiliano baina ya nchi yetu na nchi hizo jirani.
Mhandisi Ngonyani amesema kwa kutumia njia ya majini yaani Ziwa Tanganyika wafanyabiashara wataweza pia kusafirisha bidhaa zao na kuwapunguzia gharama na usumbufu waliokuwa wakiupata hapo awali.
Amesema kutokana na barabara hiyo kupita wilaya ya Kalambo, pia itachochea maendeleo kwa wananchi kwani wataweza kufanya biashara ndogo ndogo na za nyumba za kulala wageni kwa kuwa madereva na abiria wengine watalazimika kulala katika mji wa Matai ambao ni makao makuu ya wilaya ya Kalambo sambamba na mji wa Kasanga wakati wakisubiri taratibu za kuruhusu mizigo yao kwenda katika nchi hizo.
Naibu waziri huyo amewaasa wakazi wa Matai kujituma zaidi katika kuzalisha mazao ya chakula kwani barabara hiyo itakuwa  neema kwao na wataweza kuuza vyakula na kujipatia kipato kitakachowasaidia kuwekeza kwa maisha yao ya baadaye sambamba na kuwasomesha watoto wao kwa kuwapa urithi wa elimu.
Kwa upande wake Sewede Kalimalwendo, mkazi wa mji wa Matai ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo kwani kwa miaka mingi wamekuwa wakihangaika kutokana na kutokuwa na barabara ya uhakika.
Amesema barabara hiyo ya kiwango cha lami pamoja na kuwa bado haijakamilika lakini tayari wamepata manufaa makubwa ikiwemo kushuka kwa gharama za nauli, kusafiri kwa muda mfupi sambamba na kuwezesha wafanyabiashara wengine wenye mitaji mikubwa kufika katika mji wao na hivyo kununua bidhaa kwa bei nzuri tofauti na ilivyokuwa awali.