Wafanyabiashara wa Kichina wapewa semina ya ulipaji kodi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa somo la masuala ya kodi kwa wafanyabiashara kutoka China wanaoishi nchini kwa lengo la kuwaongezea uelewa juu ya sheria na taratibu za ulipaji kodi.

Akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo leo, Meneja wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Gabriel Mwangosi amesema kuwa Tanzania ya sasa ina fursa nyingi za uwekezaji hivyo wafanyabiashara hao watakapokuja kuwekeza lazima wafahamu kanuni na taratibu za ulipaji kodi nchini ili waweze kuendana na sheria zilizopangwa na nchini.

“Semina hii mahususi imeandaliwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa kichina wanaoishi nchini kupata mafunzo ya kodi zikiwemo za zuio, majengo pamoja na ushuru na forodha ambazo ni lazima wazifahamu kwa manufaa ya Taifa letu na wao pia,”amesema Mwangosi.

Mwangosi ameongeza kuwa hii ni mara ya sita kufanyika kwa semina hizo kwa wafanyabiashara hao ambapo tangu zianze kufanyika zimewasaidia kutokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa nchini.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dotto Stanley amesema kuelimisha umma hasa kwa wageni kutoka nje ya nchi ni jambo la msingi litakalowarahisishia kufahamu sheria za nchi ambapo kwa namna nyingine itachochea uwekezaji.

“Kwa kawaida wafanyabiashara wakubwa huwa wanahitaji kufahamu sheria na taratibu za nchi husika kabla hawajaamua kuwekeza mahali hivyo mafunzo hayo yatachochea uwekezaji nchini kwa sababu watakuwa na uelewa wa mchakato mzima juu ya sheria za uwekezaji na kodi.”amesema Stanley.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd, Anne Maneno amesema kuwa changamoto kubwa inayowapata wafanyabiashara wa kichina ni kukosa uelewa juu ya jinsi ya kuwekeza nchini hasa katika suala la ulipaji kodi.

“Changamoto hiyo inawapelekea wafanyabiashara kukosa muelekeo wa biashara waliyopanga kufanya kwani wengi wao wakifika Tanzania hubadilisha biashara baada ya kufahamishwa sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu biashara hivyo semina hiyo itawapa uelewa utakaowawezesha kuchagua biashara watakayoweza kuifanya kulingana na mtaji wa mfanyabiashara husika,”amesema  Anne.