Wafanyabiashara waandamana hadi kwa DC

Mkuii wa Wilaya ya Nyamagana, Mery Tesha.

Muktasari:

Maandamano hayo yamefanyika zikiwa zimepita siku sita tangu Mkuu wa Wilaya hiyo, Mery Tesha kuwaamuru kuondoka ifikapo Desemba 2 na kuhamia kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara zao.

Mwanza. Wafanyabiashara ndogondogo wakiwamo mamalishe na wauza mbogamboga na matunda wameandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyamagana wakipinga kuondolewa katikati ya Jiji la Mwanza.

Maandamano hayo yamefanyika zikiwa zimepita siku sita tangu Mkuu wa Wilaya hiyo, Mery Tesha kuwaamuru kuondoka ifikapo Desemba 2 na kuhamia kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara zao.

Wafanyabishara hao wa maeneo ya Asante Moto, Darajani, Makoroboi, Libert, Dampo, Sahara, kituo cha mabasi cha Tanganyika, Igoma na Mtaa wa Sokoni wameamriwa kuhamia katika maeneo yaliyotengwa ya Kituo cha Mabasi cha Buzuruga, Nyegezi, Sinai na Kiloleli.

Wakizungumza na gazeti hili juzi walisema watahamia katika maeneo hayo, lakini hawajaona sehemu za kufanyia kazi zao.

Mfanyabiashara Mwikabe Marwa alisema viongozi wanawahamisha kwenye maeneo hayo wakati Rais John Magufuli alitaka wamachinga wasiondolewe.

Mfanyabiashara mwingine, Mariam Abdalah aliomba wapewe miezi mitatu ya kufanya biashara hizo huku Serikali ikiwatafutia maeneo mengine ambayo ni rafiki hasa kwa mamalishe.

“Hatuna tatizo na uamuzi wa Serikali yetu ila tunachoomba ni kupatiwa maeneo rafiki tunayoweza kuuza biashara zetu na kuwafikia watu kwa ukaribu,” alisema.

Wafanyabiashara hao walimuomba Mbunge wa Nyamagana, Stansilaus Mabula kuingilia kati suala hilo kwa kuwa wao ndiyo waliopeperusha bendera ya CCM.

Alisema wengine ni wajane na wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) hivyo kupitia biashara wanajipatia kipato.

“Binafsi nilipeperusha bendera ya CCM nikijua ndiyo mkombozi wa wanyonge, viongozi walituahidi kutulinda na kututetea, leo tunaondolewa mjini hatuna pa kwenda, tunaomba Mkuu wa Mkoa, John Mongella na Rais Magufuli waingilie kati suala hili,” alisema Marwa.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.

Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Zabeda Kimaro aliyefanya mazungumzo na wafanyabiashara hao alisema: “Unataka nini mwandishi, si umeona wameondoka? Kawaulize wamejadiliana nini, sisi hatuna majibu unavyotuuliza ndivyo unavyozidi kutuchanganya. Si wamekutana na wametawanyika kawahoji wameamuaje.”

Kiongozi wa Wamachinga Mkoa wa Mwanza, Zuena Mahamudu alisema baada ya kuonana na uongozi wa wilaya hiyo wametakiwa waandae muhtasari na kuupeleka.