Wafanyabiashara wafunguka, JPM apokea kero zao

Muktasari:

Kabla ya kuanza majadiliano hayo, Rais Magufuli  amesema leo  utafanyika mjadala wa kuleta mabadiliko ambapo kila mfanyabiashara atasimama na kueleza kero na changamoto zinazomkabili

Dar es Salaam. Wafanyabiashara na wawekezaji nchini wameeleza kero na changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa shughuli zao, huku wakibainisha kuwa zimekuwa zikirudisha nyuma dhamira ya Serikali katika kukuza sekta binafsi nchini.

Wametoa kauli hizo leo Jumatatu Machi 19, 2018 Ikulu Dar es Salaam katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, huku hoja zao zikichukuliwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.

Kabla ya kuanza majadiliano hayo, Rais Magufuli  amesema leo  utafanyika mjadala wa kuleta mabadiliko ambapo kila mfanyabiashara atasimama na kueleza kero na changamoto zinazomkabili, zitapatiwa majibu na watendaji wa Serikali, wakiwemo mawaziri.

“Leo kuna watu kama 13 kutoka Tume ya Mipango, nataka tuzungumze leo kwa uwazi, mimi hata tungezungumza leo na kesho sawa tu tuendelee , nataka mseme kwa uwazi, dakika tatu kila mmoja atazungumza , nataka tu-solve problem sio kila mara tunakutana hapa tunajadili mambo yaleyale,”amesema Rais Magufuli.

Mfanyabiashara Mwita Gachuma kutoka Mwanza ndiye ameanza kufungua mjadala huo akitoa kero mbili ikiwamo tozo kubwa zinazotozwa nchini ikilinganishwa na nchi jirani kama Kenya.

 “Kwa nchi za jirani wanatoza kuanzia asilimia 11, 13, sisi (Tanzania) tunatozwa asilimia 33, asilimia 15 tunatakiwa kurudishiwa lakini hata hivyo haturudishiwi hiyo asilimia 15, hatua hiyo inaathiri hata mzunguko wetu wa fedha,”amesema.

Mfanyabiashara mwingine kutoka Geita aliyejitambulisha kwa jina moja la Sospeter amezungumzia pia kero ya kodi katika usafirishaji wa bidhaa.

Amesema TRA imekuwa ikikadiria kodi kubwa tofauti na kiwango cha mzigo.

“Kwa mfano gunia la kilo 100 unaambiwa ni zaidi ya kilo 100. Kwa hivyo inaathiri sana na matokeo yake unajikuta mfanyabiashara unabeba mzigo kidogo, kwa hiyo tunaomba ulitazame hilo,”amesema.