Monday, October 24, 2016

Wafanyabiashara wamtajia JPM kero saba zitakazomkwamisha

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfumo wa ukusanyaji kodi na tozo mbalimbali nchini, umebainika kuwa kero namba moja miongoni mwa saba zilizotajwa na viongozi wafanyabiashara ambazo huenda zikamkwamisha Rais John Magufuli kufikia ndoto ya viwanda.

Utafiti huo unaonyesha kero nyingine zinazowatesa wafanyabiashara ni uhaba au ukosefu wa huduma ya umeme, makato makubwa ya kiwango cha kodi, rushwa, ukosefu wa mitaji na ubovu wa barabara.

Wafanyabiashara hao walisema utitiri wa kodi usiokuwa na mpangilio au usiotambuliwa rasmi umekuwa ukiwakatisha tamaa kuendeleza au kukuza biashara zao.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), uliopewa jina la Mtazamo wa Viongozi Wafanyabiashara Juu ya Mazingira ya Uwekezaji Tanzania 2015, unaonyesha kati ya viongozi wafanyabiashara 597 waliohojiwa, nusu walisema biashara zinakabiliwa na kikwazo cha ukusanywaji wa kodi unaofanywa na halmashauri na taasisi za Serikali.

Utafiti huo ulifanyika kati ya Agosti na Septemba, 2015 katika mikoa mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema: “Tulipowauliza sababu (wafanyabiashara hao) wakasema siyo kwamba hawataki kulipa kodi, ila walilalamikia zile zisizokuwa na utaratibu maalumu, wakapendekeza kwa nini kusiwapo na mfumo unaozitambua tozo na kodi wanazotakiwa kulipa.”

Hata hivyo, Simbeye alisema matokeo ya utafiti huo hayahusiani na uongozi uliongia madarakani Novemba mwaka jana.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Hussein Kamote alisema Serikali inaweza kuchelewa kufikia ndoto ya viwanda endapo haitabadilisha mfumo wa makusanyo ya tozo kwa mamlaka zinazofanya kazi zinazofanana.

“Kwa mfano Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango (TBS), halafu Osha (Wakala wa Usalama na Afya Sehemu za Kazi) na Zimamoto wanatoa huduma zinazofanana, lakini kila moja inataka tozo kwa mmiliki wa kiwanda anayetaka huduma zao,”alisema.

-->