Wafanyabiashara watakiwa kuchangamkia fursa za msamaha wa kodi

Kaimu kamishina wa walipakodi wakubwa Alfred Mregi

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango alipendekeza msamaha huo kutolewa katika kipindi cha Julai Mosi hadi Desemba 31

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imewataka wafanyabiashara wenye madeni ya malimbikizo ya riba na adhabu za kodi, kutumia vyema fursa ya msamaha uliotolewa.

Akisoma hotuba ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipendekeza msamaha huo kutolewa katika kipindi cha Julai Mosi hadi Desemba 31.

Wito huo umetolewa leo Agosti 14 na kaimu kamishina wa walipakodi wakubwa Alfred Mregi wakati wa semina iliyotolewa na TRA kwa wafanyabiashara wakubwa iliyofanyika jijini hapa.

Mregi alimuwakilisha kamishina mkuu Charles Kichere.

Mregi amesema msamaha huo uliopitishwa katika sheria ya bajeti ya mwaka 2018/2019 unatoa fursa kwa wafanyabiashara kufutiwa malimbikizo ya kodi zao na penalti kwa asilimia 100 lakini pia unajenga mwanzo mpya wa ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara.

“Serikali ya awamu ya tano sasa inapambana kuwa imara kiuchumi na kujitegemea, suala hili linawezekana endapo kutakuwa na mazingira bora ya ufanyaji wa biashara, ulipaji kodi kwa hiari na hayo ndiyo yanayovutia ukusanyaji wa kodi za ndani,” amesema Mregi.

Anasema ushauri wake kwa wafanyabiashara wakubwa ni kuwasilisha maelezo yao na vithibiti endapo watatakiwa ili wahudumiwe haraka.

Hata hivyo Mregi amewataka maofisa wote wa TRA kuhakikisha wanatenda haki katika mchakato huo.