Wafanyabisahara walalamikia wino wa risiti za kielektroniki

Muktasari:

Kutokana na tatizo hilo, wanalazimika kuingia gharama nyingine ya kupiga kopi risiti za mauzo ili kuweka kumbukumbu zinazoweza kudumu kwa muda mrefu tofauti na zinazotoka moja kwa moja kwenye mashine hizo.

Baadhi ya wafanyabiashara jijini hapa wamedai wino unaotumika kutolea risiti kwenye mashine za kieletroniki za EFD haudumu muda mrefu, jambo linalowafanya kushindwa kutunza vizuri kumbukumbu za mauzo.

Kutokana na tatizo hilo, wanalazimika kuingia gharama nyingine ya kupiga kopi risiti za mauzo ili kuweka kumbukumbu zinazoweza kudumu kwa muda mrefu tofauti na zinazotoka moja kwa moja kwenye mashine hizo.

Mfanyabiashara kutoka Soko la Uyole, Regnet Sangwa alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapaswa kufanya uchunguzi ili kuja na suluhisho la wino unaotumika udumu kwa muda mrefu kwenye risiti hizo kabla ya kuzisambaza kwa wafanyabiashara.

“Maandishi ya risiti hizi yanafutika ndani ya muda mfupi sana, jambo linalofanya wengi wetu tushindwe kuweka kumbukumbu sahihi au tofauti na hapo inanilazimu niingie gharama nyingine kwenda kupiga kopi,” alisema Sangwa.

“Tunalazimika kufanya hivi kwa sababu muda mwingine wenzetu wa TRA wanakuja na kudai kumbukumbu za mauzo, sasa kama hukupiga kopi na zile original zinakuwa zimefutika maandishi ndio inakuwa shida, tunaambiwa tunakwepa kulipa kodi.”

Mfanyabiashara huyo alisema Serikali ilipaswa kufanya uchunguzi wa awali wa mashine hizo kabla ya kuwapelekea wafanyabishara na kwamba, zina upungufu mwingi ikiwamo kutokuwa na sehemu ya kuandika jina la mnunuzi, bali zinaandika jina la mmiliki wa biashara jambo ambalo linawapa wakati mgumu.

Mfanyabiashara mwingine, Riziki Sanga wa Uyole alisema mashine hizo zina masharti mengi katika matumizi na ni rahisi kuharibika.

Alisema mawakala wanaosambaza mashine hizo wamekuwa hawatoi elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara ya namna ya kuzitumia kwa ufanisi na kujikuta wanaziharibu mara kwa mara.

Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Charles Bajungu alisema tatizo la wino katika mashine hizo wanaliona kuwa ni changamoto kutokana na kutodumu kwa muda mrefu. Hata hivyo alisema wanalishughulikia.

“Kuna baadhi ya changamoto kwenye mashine hizo ikiwamo ya risiti kutokuwa na jina la mnunuzi pamoja na wino unaotumika kutodumu kwa muda ambao tulitarajia, lakini tunaendelea kuzifanyia marekebisho, muda si mrefu tatizo hilo litakuwa limepata ufumbuzi,” alisema.

Bajungu alisema baadhi ya wafanyabiashara wa mkoa huo wana utamaduni wa kukwepa kulipa kodi kwa kisingizio kuwa elimu haitolewi ipasavyo.

Alisema wanafanya makosa kwa kwa kuwa elimu ya mlipakodi pamoja na matumizi ya mashine za EFD imekuwa ikitolewa mara kwa mara.

Alisema mawakala wanaohusika na usambazaji wa mashine hizo muda wote wako mitaani na wamekuwa wakitoa elimu juu ya matumizi yake kabla, hivyo si kweli kwamba hawawajibiki kutoa elimu ya matumizi sahihi.