Wafanyakazi, wanachama wa Pride wamwangukia Rais Magufuli

Kaimu Meneja wa Pride kanda ya Dar es Salaam, akizungumza katika mkutano wa wafakazi na wanachama wa shirika hilo.

Muktasari:

Wanachama na  wafanyakazi shirika Pride wamuomba Rais Magufuli aingilie kati ili kuwezesha kupata haki zao baada ya shirika hilo kusuasua katika utendaji kazi.

Dar es Salaam. Wafanyakazi na wanachama wa Shirika la kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wakubwa (Pride),wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati ili walipwe fedha zao.

Wafanyakazi hao kutoka matawi 10 ya Jiji la Dar es Salaam na wawakilishi wa wanachama walikutana leo Septemba 21,2018 katika ofisi za Pride zilizopo Keko Bora jijini Dar es Salaam kuweka maazimio ya nini wafanye ili kupata haki yao.

Kaimu Meneja wa  Pride Kanda ya Dar es Salaam, Felician Primus alisema wameamua kufikia hatua hiyo baada ya muda mrefu kwenda kwa viongozi mbalimbali ikiwamo kwa Mkuu wa Mkoa bila ya mafanikio.

Primis ameyataja malimbikizo wanayoyadai ni pamoja na mishahara ambayo hawajalipwa tangu Desemba mwaka jana, fedha za likizo, rambirambi, kodi mbalimbali pamoja na michango ya NSSF ambayo wamekuwa wakikatwa lakini haifikishwi sehemu husika.

Amebainisha  matatizo katika shirika hilo yalianza kujitokeza kuanzia mwaka 2016 baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani huku wakiwa na hisia kwamba kuna ujanja ujanja uliokuwa ukiendelea ambayo usingeweza kuvumikiwa na Serikali ya awamu hii.

"Kama Serikali ilivyofanya jitihada ya kuanzisha taasisi hii, tunaomba zitumike katika kutupatia haki zetu ambazo tumezisotea kwa muda mrefu bila ya mafanikio huku baadhi ya watendaji tukiwa tunaendelea kupishana nao barabarani bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi yao za kuifikisha Pride hapa," amesema Meneja huyo.

 Mwenyekiti wa wanachama wa Pride, Emily Sanga amesema pamoja na wanachama kuwa na fedha nyingi katika matawi ya shirika hilo, mengi yameshafungwa na hawajui wapi wataenda kupata haki zao.

Sanga amesema wengi wamekopa fedha maeneo mengine wakiwa na matarajio wangepata za kurudisha kupitia shirika hilo lakini hawajafanikiwa na hivyo kukatiza ndoto za mipango ya maisha yao.

Mfanyakazi aliyejitambulisha kwa jina la Meshak Mollel amesema kukaa kimya kwa viongozi wa shirika hilo hakutawafanya wao kunyamaza kudai haki zao.

Badala yake amesema ni vyema wakajitokeza na kuwaeleza kama shirika limekufa au la kuwafafanulia na watakavyopata haki zao badala ya kuwakimbiakimbia kila wanapohitaji kuonana nao.