Wafanyakazi wa meli watangaza mgogoro

Muktasari:

  • MSCL imeshindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi hao tangu Februari, kutokana na ukata ambao umesababishwa na kuharibika kwa zaidi ya nusu ya meli zinazomilikiwa na kampuni hiyo.

Mwanza. Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (Dowuta), kimetangaza mgogoro wa kikazi dhidi ya uongozi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), kushinikiza wanachama wao kulipwa malimbikizo ya mishahara na michango yao.

MSCL imeshindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi hao tangu Februari, kutokana na ukata ambao umesababishwa na kuharibika kwa zaidi ya nusu ya meli zinazomilikiwa na kampuni hiyo.

Dowuta imetangaza mgogoro huo ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alipoliambia Bunge mjini Dodoma kuwa ofisi yake imetenga Sh50.5 bilioni mwaka kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya meli za MSCL.

“Ni kweli Dowuta tumewapa taarifa ya kusudio la kutangaza mgogoro MSCL, tunakusanya kura ili tupate uhalali wa kisheria ikiwamo kumfikisha Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA) tukishapata orodha ya wafanyakazi wanaodai mishahara na michango mingine ya kisheria,” alisema Msoma.