Wafiwa waelezea walivyofarijika na Sh1.5 milioni

Muktasari:

  • Wafiwa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere wameishukuru Serikali kwa kuwapa mkono wa pole wa Sh1.5 milioni wakisema ingawa fedha haiwezi kurejesha ndugu zao, lakini uamuzi huo umewafariji

Ukara. Wafiwa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere wameishukuru Serikali kwa kuwapa mkono wa pole wa Sh1.5 milioni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Septemba 26, 2018 baada ya kupokea nyongeza ya fedha taslimu Sh1 milioni baadhi ya wafiwa wamesema japo hakuna kiwango cha fedha kinachoweza kuziba pengo la kuondokewa na wapendwa wao, uamuzi huo wa Serikali umewafariji.

"Kiwango chochote cha fedha hakiwezi kurejesha maisha ya watoto wangu wawili waliokufa kwenye ajali; lakini nimefarijika kuona Serikali imetujali kwa kutoa mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila marehemu," amesema Mzee Stanslaus Mpungu aliyefiwa na watoto wawili

Licha ya kushukuru, mfiwa mwingine, Revocatus Machere ameiomba Serikali kuongeza udhibiti na usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji majini ikiwemo lile la vyombo vya kupakia abiria na mizigo kulingana na uwezo.

"Idadi ya abiria kwenye vyombo vya majini iwe kama inavyofanyika kwenye vyombo vya nchi kavu na angani," amesema Machere

Kwa upande wake, Dk Fred Mtoroki aliyepoteza mama yake mzazi na mdogo wake katika ajali hiyo ameishauri Serikali kuimarisha vitengo vya uokoaji kwa kununua zana, vifaa na kuwajengea uwezo wataalam wa kitengo hicho.

"Silaumu wala kunyooshea mkono mtu au taasisi kwa ajali hii maana yameshatokea. Lakini ni vema tukatumia funzo hili kijipanga kwa kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga," amesema Dk Mtoroki ambaye ni daktari wa binadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi ambaye pia ni mkazi wa Kisiwa cha Ukara naye ameungana na wapiga kura wake kuishukuru Serikali kwa kutoa mkono wa pole kwa wafiwa na walionusurika katika ajali hiyo.

Wakati wafiwa wamepewa Sh1.5 milioni kwa kila marehemu, walionusurika kila mmoja amepewa Sh1 milioni.