Tuesday, January 30, 2018

Wafugaji 480 Arusha kufundishwa Kiingereza

Mwalimu John Macha akiwafundisha lugha ya

Mwalimu John Macha akiwafundisha lugha ya Kiingereza baadhi ya wajasiriamali wa jamii ya kimasai, baada ya taasisi ya Chemchem kuwalipa walimu ili kutoa elimu hiyo kwa wajasiriamali 480 katika vijiji 10 vilivyopo eneo la Hifadhi ya Tarangire. 

By Mussa Juma,Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz

Arusha. Wajasiriamali 480 wa jamii ya wafugaji wanaouza bidhaa kwa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Tarangire, wameanza kufundishwa lugha ya kiingereza ili waweze kuwasiliana na wageni hao, badala ya kutumia wakalimani.

Mafunzo hayo yanatolewa na taasisi ya Chemchem katika vijiji 10 vilivyopo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Burunge (WMA).

Akizungumza leo Januari 30, mwaka 2018 meneja wa taasisi hiyo, Charles Sylivesta amesema mafunzo yatafanyika kwa miezi miwili katika kila kijiji, awamu ya kwanza itagharimu zaidi ya Sh100milioni ambazo taasisi hiyo itawalipa walimu wanaowafundisha wajasiliamali hao.

Amesema wajasiriamali 48 katika kila kijiji watafundishwa lugha hiyo.

"Tayari tumetoa mafunzo kijiji cha Mdori, sasa mafunzo yanaendelea kijiji cha Kakoi na baadaye watafundishwa wananchi wa Sangaiwe na hii ni awamu ya kwanza awamu nyingine zitafata katika vijiji vyote,"amesema.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wajasiriamali hao wamesema  lugha hiyo itawasaidia kuwasiliana na watalii, kurahisisha ufanyaji wa biashara.

Raheli Hagai amesema walikuwa wanalazimika kutumia mkalimani kuzungumza na watalii ili kuuza bidhaa zao kama shanga na vikapu.

"Tumejifunza kusalimiana na wageni, kuwaeleza bei ya bidhaa na majina ya bidhaa zetu na hata kuwaelekeza njia za kupita,” amesema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kakoi, Daniel Merita amesema mafunzo hayo yatasaidia kuwaepusha na utapeli uliokuwa ukifanywa na wakalimani kwa sababu ya kutojua kiingereza.

“Walikuwa wanawatapeli kwa kuwapa pesa kidogo  licha ya watalii kutoa fedha nyingi kwa kuwa wao ndio walikuwa wanapatanisha biashara lakini sasa watafanya wenyewe biashara,” amesema.

 

-->