Wafugaji Njombe waomba Serikali kuingilia bei ya pembejeo

Muktasari:

  • Katika mkakati wa kuongeza faida na kukuza sekta ya ufugaji, wafugaji mkoani Njombe wameomba kupunguzwa kwa bei ya pembejeo za mifugo pamoja na kuimarishwa kwa masoko ya maziwa.

Njombe. Siku chache baada ya kuanza kutumika kwa kanuni mpya za huduma za mifugo zilizopandisha tozo ya maziwa na bidhaa zake kutoka nje ya nchi, wafugaji wa ng`ombe wa maziwa mkoani Njombe wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za pembejeo ili kuongeza uzalishaji.

 

Licha ya bei ya pembejeo vilevile wameiomba Serikali kusimamia mauzo ya bidhaa za mifugo yafanyike kwa kutumia vyama vya ushirika kama ilivyo kwenye mazao ya kilimo.

 

Maoni hayo yametolewa na wafugaji wa Kijiji cha Itulike Kata ya Ramadhani mkoani hapa walioeleza kuwa sekta ya maziwa inahitaji usimamizi ili kuongeza tija kwa wafugaji nchini.

 

Mmoja wa wafugaji hao, Deborah Zacharia anayefuga ng`ombe wa kisasa kwa zaidi ya miaka 10 sasa, amesema mafunzo na ushauri wa kitaalamu wanaoupata kutoka Shirika la Heiffer International linalotekeleza mradi wa uendelezaji wa maziwa Afrika Mashariki (EADD) umeimarisha uzalishaji wao.

 

“Tunazalisha hadi lita 50 kwa siku lakini hatuwezi kukidhi mahitaji kwa sababu bei ya pembejeo ipo juu. Tunaiomba Serikali itusaidie kuliangalia suala hili,” amesema Deborah.

 

Kuimarisha masilahi ya wafugaji, ameshauri uandaliwe utaratibu utakaokuwa unakusanya maziwa kutoka kwa wakulima wengi ambao wataweza kuchanga kiasi kidogo kupitia ushirika ili kununua pembejeo kwa bei ya jumla ili kuwapa unafuu.

 

“Licha ya mauzo ya rejereja kuna kiwanda cha Asas ambacho kinahitaji mzigo mkubwa, ushirika ndio utakaotusaidia  kunufaika na soko hilo huku tukipunguza gharama za uendeshaji,” amesema mfugaji huyo.

 

Mfugaji mwingine, Obeid Kusima anayetoka Chama cha Ushirika cha Mshikamano amesema bei ya pembejeo mfano dawa za kuogesha na kutibu mifugo kama vile ng`ombe ndizo zinazowaumiza zaidi.

 

“Tukijunga kwenye vikundi vya ushirika inakuwa rahisi kupata elimu ya ufugaji hivyo kukabiliana kwa urahisi na changamoto zitakazojitokeza,” amesema Kusima.

 

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepitisha kanuni mpya ambazo zinawataka waingizaji wa maziwa kulipia Sh5,000 kwa kila kilo au lita moja watakayoiingiza kutoka nje ya nchi.